Shirika la Kimataifa la kutetea haki za binadamu, katika ripoti yake, kuhusu vurugu zilizotokea nchini Tanzania, siku ya upigaji kura Oktoba 29, imesema polisi walitumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji na kuhusika katika visa vingine vya ukiukwaji wa haki za binadamu.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Human Rights Watch imesema polisi walitumia risasi kuwashambulia waandamanaji waliojitokeza kwenye miji mbalimbali hasa Dar es salaam, kupinga kufanyika kwa uchaguzi huo.
Oryem Nyeko, mtafiti wa Shirika hilo, kwenye ripoti yake, amesema machafuko yaliyotokea na namna waandamanaji walivyokabiliwa kwa nguvu, hali hiyo inatia doa uhalali wa uchaguzi huo.

Rais Samia Suluhu Hassan, aliapishwa siku ya Jumatatu, kuongoza kwa muhula wa pili, baada ya Tume ya Uchaguzi kumtangaza mshindi kwa kupata asilimia 98 ya kura, matokeo ambayo chama kikuu cha upinzani CHADEMA, kimekataa na kusema ushindi wake ni kichekesho kwa demokrasia.
Aidha, katika ripoti yake, Human Rights inaitaka serikali ya Tanzania, kuheshimu na kulinda haki za msingi za wananchi, za kujieleza, kukusanyika kwa amani kama inavyotakiwa na sheria za kimataifa za haki za binadamu na katiba ya nchi hiyo.

Rais Samia amemshtumu machafuko yaliyotokea, na kudai kuwa baadhi ya vijana waliokamatwa kwenye maandamano hayo ni raia wa kigeni, huku chama cha CHADEMA kikisema kimenakili vifo vya karibu watu 1,000 kupitia mkurugenzi wake wa mambo ya nje John Kitoka, lakini Human Rights Watch inasema haijathibitisha idadi hiyo, huku waangalizi wa Kimataifa wakiongozwa na wale kutoka Jumuiya ya SADC wakisema uchaguzi wa Tanzania, haukufikia viwango vya demokrasia.