Serikali ya Tanzania yakabiliwa na shinikizo zaidiSerikali ya Tanzania yakabiliwa na shinikizo zaidi

Maandamano ya kupinga Uchaguzi wa Oktoba 29 yalishuhudiwa kwa siku kadhaa katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania huku vijana wakiingia mitaani katika miji ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na mahali pengine ili kupinga kile walichotaja kwamba halikuwa zoezi la huru wala haki.

Vikosi vya usalama vilijaribu kuyazima maandamano hayo kwa kutumia mabomu ya machozi na hata kuwafyatulia waandamanaji risasi za moto huku amri ya kutotoka nje usiku ikitangazwa nchini humo. Brenda Rupia, mkuu wa kitengo cha mawasiliano wa chama cha upinzani CHADEMA ameliambia shirika la habari la AP kwa njia ya simu kuwa kwa sasa mioyo ya Watanzania inavuja damu na kwamba hili ni jambo jipya kwao.

Alipoulizwa ikiwa familia za wahanga wa maandamano hayo zimeweza kufanya mazishi, Bi Rupia amesema vikosi vya usalama “vinazuia maiti” na kwamba baadhi ya miili imekuwa ikizikwa kwa siri na vikosi hivyo ili kuficha ukubwa wa mauaji hayo.

Kumekuwa na ripoti juu ya vifo vingi kufuatia maandamano hayo. Wiki iliyopita, chama cha upinzani CHADEMA kilisema watu wasiopungua 700 waliuawa katika siku tatu za vurugu zilizoshuhudiwa wakati na baada ya uchaguzi, taarifa ambazo zilikanushwa vikali na serikali ya Tanzania ambayo hata hivyo haijatoa idadi rasmi ya waliofariki.

Tanzania Dar es Salam 2025 | Maandamano ya kupinga Uchaguzi Mkuu wa Tanzania, Oktoba 2025
Maandamano ya kupinga Uchaguzi Mkuu wa Tanzania, Oktoba 2025Picha: Onsase Ochando/REUTERS

Mataifa kama Uingereza, Norway na Canada, yametaja uwepo wa ripoti za kuaminika za idadi kubwa ya vifo huku Kanisa Katoliki likisema kuwa “mamia ya watu” walikufa ingawa pia halikuweza kuthibitisha idadi kamili.

HRW lalaani ukandamizaji

Kwa upande wake, Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limelaani vitendo vya ukandamizaji dhidi ya waandamanaji na kuitaka mamlaka ya Tanzania “kukomesha” matumizi ya nguvu kupita kiasi na kuchukua hatua za kuhakikisha uwajibikaji wa vikosi vya usalama.

Katika hotuba yake siku ya kuapishwa, Rais Samia Suluhu Hassan alikiri kutokea vifo na alivihimiza vyombo vya usalama kuhakikisha hali ya kawaida inarejea huku akitoa wito wa kuzingatia umoja, amani na mazungumzo.

” …Ndugu zangu, wote tunalitakia taifa hili mema, na tunasikitishwa sana na matukio ya vurugu ambayo yamesababisha vifo na uharibifu wa mali za umma na zile za watu binafsi katika baadhi ya maeneo ya nchi yetu,…” alisema Rais Samia.

Ghasia za baada ya uchaguzi Tanzania,Mtihani kwa rais Samia

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Wakati mawasiliano ya intaneti yakirejea baada ya kukatwa kwa karibu wiki nzima, mamlaka imewaonya watanzania kutosambaza picha na video zinazoweza kusababisha hofu ikisema kuwa vitendo hivyo vinaweza kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria.

Rais Samia Suluhu Hassan alitangazwa mshindi kwa zaidi ya asilimia 97 ya kura na tayari ameapishwa. Lakini ushindi huo wa kishindo unapingwa vikali na upinzani, huku waangalizi wa kigeni wakisema kuwa idadi ya walioshiriki uchaguzi huo ilikuwa ndogo. Ushindi huo tata wa rais Samia umezidisha pia ukosoaji kuwa uchaguzi huo haukuwa wa kuaminika.

Wapinzani wake wakuu ambao ni Tundu Lissu wa CHADEMA na Luhaga Mpina wa ACT-Wazalendo hawakuweza kugombea urais. Lissu yupo gerezani kwa miezi kadhaa sasa, akikabiliwa na mashtaka ya uhaini kufuatia wito wake wa kufanyika mageuzi makubwa kwenye mfumo mzima wa uchaguzi. Naibu wake, John Heche, alikamatwa pia siku chache kabla ya uchaguzi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *