
Dar es Salaam. Maumivu, wasiwasi na mashaka, ndiyo uhalisia wa kile walichokipitia wakazi wa baadhi ya mikoa nchini ikiwemo Dar es Salaam, katika siku sita za matukio ya vurugu na uvunjifu wa amani yaliyosababisha mabadiliko ya mtindo wa maisha.
Matukio hayo yaliyotokea kuanzia Jumatano, Oktoba 29, 2025, yalihusisha baadhi ya wapinzani wa Serikali, kuandamana na kuchoma moto baadhi ya miundombinu vikiwemo vituo vya polisi, ofisi za Serikali za mitaa, vituo vya mabasi yaendayo haraka, vituo vya mafuta, maduka na magari.
Hatua hiyo ilisababisha Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania, Camilius Wambura, kutangaza amri ya wakazi wa Dar es Salaam kutotoka nje kuanzia saa 12 jioni, huku shughuli za kijamii pia zikizuiwa kama hatua ya tahadhari dhidi ya kilichokuwa kinaendelea.
Marufuku hiyo ilisababisha kubadilika kwa mtindo wa maisha ya wananchi, wengi wakisimulia maumivu, wasiwasi na mashaka walioyapitia kwa siku sita za kukaa ndani bila kwenda popote, huku kukiwa na hali ngumu ya upatikanaji wa huduma za jamii.
Ilivyokuwa
Vurugu hizo katika Jiji la Dar es Salaam zilianzia eneo la Kibo na Ubungo Maji, muda wa upigaji kura kwa ajili ya uchaguzi mkuu. Kundi la vijana wa rika tofauti lilishuhudiwa likiifunga Barabara ya Morogoro kwa mawe na magogo.
Polisi waliokuwepo mitaani kuimarisha ulinzi na kuhakikisha usalama siku ya uchaguzi, waliwatawanya vijana hao kwa mabomu ya machozi na kundi hilo kujibu mashambulizi kwa kurusha mawe.
Wakati polisi wa kutuliza ghasia wakidhibiti eneo hilo, vurugu zilihamia eneo la Ubungo Mataa, kisha Shekilango na kusambaa maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam.
Haikuchukua muda, waandamanaji walionekana wakivamia vituo vya mabasi yaendayo haraka na kuvichoma moto, huku vingine wakiishia kuvunja mageti janja na vioo.
Hali kama hiyo ilishuhudiwa katika vituo vya mafuta, ambapo waandamanaji walivamia baadhi ya vituo hivyo na kuvichoma moto sambamba na magari yaliyokuwepo vituoni humo.
Haukuishia hapo, baadhi ya vituo vya upigaji kura vilikumbwa na msukosuko huo, kwani waandamanaji walivichoma moto na wakati mwingine kusambaratisha vifaa vilivyotumika kuhifadhia karatasi za kura na kura zenyewe.
Katika Barabara ya Morogoro na nyingine, ilikuwa haramu kwa mwananchi kupita na chombo cha usafiri. Kila aliyepita walipo waandamanaji, walishushwa na kushurutishwa kuungana nao. Aliyegoma, usafiri wake ulichomwa moto.
Katika Barabara ya Mandela, waandamaji walichoma moto kituo cha polisi, ofisi ya Serikali za mtaa, vituo vya mafuta. Katika barabara ya Nyerere, waliharibu vituo vya mabasi ya mwendokasi na kuchoma jengo zilizopo ofisi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) eneo la Vingunguti.
Maandamano hayo yaliendelea hadi kwenye maduka ya baadhi ya watu maarufu. Baadhi yalivamiwa na waandamanaji kuingia ndani, kuchukua kilichokuwemo kisha kuyachoma moto.
Mpaka kufikia saa 9 alasiri ya Oktoba 29, hali ya usafiri jijini Dar es Salaam ilikuwa tete, matairi yakiwa yamechomwa katikati ya barabara na kilichokuwa kikisikika ni milio ya mabomu ya machozi na bunduki za kuwatawanya waandamanaji.
Mmoja wa mashuhuda, Wema Masatu (si jina lake halisi), ameiambia Mwananchi namna walivyopata ugumu kutoka Tabata Relini hadi Mbezi, wakipita njia tofauti kabla ya kushambuliwa Kimara Temboni.
“Nilipata lifti nikiwa natoka ofisini. Kwenye gari yetu tulikuwa wanne, kila njia tuliyopita hatukufanikiwa kufika mwisho. Tulirudishwa na wasamaria wema waliotushauri tutafute njia nyingine, na tukafanikiwa kupita Bonyokwa hadi kutokea Kimara Mwisho,” amesema.
Amesema njiani kote walikuta vituo vingi vya kupigia kura, baadhi ya vituo vya mafuta na magari vikiwa vimechomwa.
“Tulipofika Suka tukaambiwa huko mbele hakufai, turudi. Tukawa njia panda, tunakokwenda ni mbali na tulikotoka ni mbali zaidi.
“Ikabidi tujaribu kurudi Barabara ya Morogoro, ambako kulikuwa na magari kama sita hivi yenye eskoti ya polisi waliokuwa wakifyatua risasi kutawanya makundi ya vijana,” amesema.
Amesema barabara ilikuwa imechafuliwa kwa matairi yaliyochomwa, wakati huo yadi ya magari iliyokuwa jirani ikiwa imeunguzwa, na pembeni yao kulikuwa na lori la mafuta lililochomwa, moto ukiwa umeanza kushika kwenye matairi.
“Licha ya eskoti ya polisi, waandamanaji hawakujali. Waliingia barabarani na kuanza kuturushia mawe, gari yetu iliharibiwa vibaya.
“Tulipofika Mbezi Darajani hali ilikuwa mbaya zaidi. Pale kulikuwa na magari ya polisi kama matatu na polisi zaidi ya 20 wenye bunduki na mabomu ya machozi wakipiga, lakini waandamanaji hawakuondoka, walipambana kwa kurusha mawe.
“Ilikuwa kubaki kwa polisi ni hatari, kwenda kwa waandamanaji nako ni hatari. Nakumbuka bosi wetu, ambaye alitupa lifti na ndiye alikuwa dereva, alituambia ‘tumefika uwanja wa vita, kila mmoja asali kwa imani yake,’” amesema Wema.
Kauli ya IGP
Ilipofika saa 10 alasiri, IGP Wambura alitangaza marufuku ya wakazi wa Dar es Salaam kutotoka nje kuanzia saa 12 jioni. Pia, wale wasio na ulazima wa kutembea barabarani watulie nyumbani.
Katika taarifa yake hiyo, alisema ni askari wa jeshi hilo na vyombo vingine vya ulinzi na usalama pekee ndio wanaoruhusiwa kuwepo nyakati hizo kwa ajili ya operesheni maalumu.
Kauli hiyo ilifuatiwa na ile ya Katibu Mkuu Kiongozi, Moses Kusiluka, aliyewataka watumishi wa umma wote kufanyia kazi nyumbani Oktoba 30, isipokuwa wale ambao kazi zao zinalazimu wawepo ofisini.
Agizo hilo liliwahusu pia wafanyakazi wa sekta binafsi, huku Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ikitangaza likizo fupi kwa wanafunzi wa ngazi zote na kusogeza mbele kwa wiki moja ratiba ya mitihani ya taifa ya kidato cha pili na nne.
Maumivu ya Lockdown
Hali ilikuwa mbaya zaidi hasa kwa wananchi ambao kula yao ilitegemea kibarua cha siku. Wengi hawakuwa na akiba wala bakaa, huku shughuli za kuwaingizia kipato zikisimama.
Matumaini yalizidi kupotea kadiri milio ya bunduki na mabomu ya kuwatawanya wananchi ilivyoendelea kusikika, kwani ilijulikana lini maandamano yalianza, lakini haikujulikana lini yangemalizika.
Ukiacha waliokosa akiba ya fedha na bakaa ya chakula, wapo wenye fedha katika mitandao ya simu na benki, nao walijikuta wakiishi sawa na wale wasiokuwa na chochote.
Hiyo ilitokana na ukweli kwamba hakukuwa na wakala wa kutoa fedha kwa mitandao ya simu, wala tawi la benki lolote lililokuwa wazi kutoa huduma za kifedha. Kila huduma ilifungwa.
Ile methali ya kuvuja kwa pakacha nafuu ya mchukuzi iliakisi uhalisia. Wenye maduka na magenge waliitumia hali hiyo kama fursa, wakipandisha bei ya bidhaa hasa muhimu ikiwemo chakula.
Eneo la Ubungo, kiungo kama nyanya hakikuuzwa kwa mafungu bali moja moja kwa Sh500, huku Kinondoni nyanya moja ikiuzwa Sh1,000.
Pia nauli ya bodaboda itakushangaza. Eneo lililogharimu Sh1,000 kwa usafiri huo, gharama ilipanda hadi Sh 5,000. Hiyo ilitokana na kupanda kwa bei ya mafuta kutoka takriban Sh 3,500 kwa lita hadi Sh 10,000.
Hata hivyo, mafuta hayo hayakuuzwa kwenye vituo rasmi bali yalikuwa yakipitishwa kwenye madumu, wengine wakiwa wameshayapima na kuyahifadhi katika chupa za lita moja moja.
Yote hayo yametokana na kufungwa kwa vituo vya mafuta baada ya kadhaa kuchomwa moto na waandamanaji. Hali hiyo ilisababisha baadhi ya madereva wa bodaboda washindwe kufanya kazi hata katika maeneo yaliyokuwa na uwezekano wa kusafirisha abiria.
Wapo waliobakiza chini ya nusu lita kwenye pikipiki zao, ilimradi yawasaidie kufika vituo vya mafuta siku hali itakapotulia, kama alivyoeleza Emmanuel Mathias, dereva bodaboda wa Kimara Korogwe, Dar es Salaam.
“Mafuta yaliyobaki yananiwezesha kufika kituo cha mafuta pale huduma zitakapofunguliwa. Nimeshakaa siku tatu sijafanya kazi kwa sababu sina mafuta na hali haijatulia. Nimeishiwa fedha ya matumizi sijui nifanyeje,” amesema Mathias.
Wakati hali ikiwa hivyo kwa Mathias, Issa Zahoro anayefanya shughuli hiyo pia amesema amebahatika kupata lita mbili za petroli alizonunua kwa Sh 20,000 kutoka kwa muuzaji wa mtaani, si kituo cha mafuta.
“Hapa hakuna safari ya Sh 1,000 au Sh 2,000. Safari hata iwe fupi kiasi gani, nauli yake inaanzia Sh5,000. Ndio namna pekee itakayonipa faida kutokana na gharama ya mafuta,” amesema.
Hali ilikuwa mbaya kwa sababu hata ungeumwa, hakukuwa na namna ya kupata huduma za matibabu, kwani si maduka ya dawa wala zahanati na vituo vya afya vilivyokuwa wazi hasa jijini Dar es Salaam.
Zilizokuwa wazi ni hospitali za wilaya za baadhi ya taasisi za umma likiwemo Jeshi la Ulinzi na Hospitali ya Taifa Muhimbili. Hata hivyo, haikuwa rahisi kuzifikia kwa kuwa barabarani ndiko walikokuwepo waandamanaji.
Ingawa waandamanaji walidai dhamira yao ni kudai haki ikiwemo utawala bora na kudhibiti ubadhirifu wa mali za umma, lakini wenyewe ndio waliokuwa wakichoma miundombinu ya umma, vikiwemo vituo vya mabasi yaendayo haraka na vituo vya mafuta.
Walishangaza zaidi hasa pale walipokuwa wanachoma hata magari na pikipiki za wananchi kila walipoziona barabarani. Kwa maneno mengine, waandamanaji walikuwa hatari zaidi kwa raia kuliko kitu kingine chochote.
Wapo baadhi ya wafanyabiashara waliokuwa wakifungua maduka mithiri ya wauza magendo. Wengine walijificha ndani ya maduka na ukihitaji huduma, ilikubidi kubisha hodi, anathibitisha kisha anakuhudumia kwa kificho.
Katika baadhi ya mitaa ya Tabata- St. Marys, wananchi walishindwa kupata baadhi ya mahitaji ikiwemo mafuta ya kupikia, huku bei za bidhaa za vyakula zikiongezeka kwa zaidi ya nusu, jambo lililowaathiri wananchi.
Hiyo ni kwa sababu wananchi walilazimika kutumia fedha zaidi ili kupata milo yao ya kila siku, wakati ambao hawakuingiza kipato chochote.
“Nyama ni Sh 20,000 kilo. Huko machinjioni hazipatikani kwa urahisi, bei imeongezeka kwa sababu mifugo hailetwi na inayochinjwa ni ile iliyokuwapo tayari,” amesema Chacha Mashinji, mfanyabiashara wa bucha.
Mbali na nyama, mahitaji mengine kama mikate, mchele na mafuta ya kupikia yote yaliadimika, hali iliyofanya watu kutembea umbali mrefu kutafuta licha ya kuhatarisha usalama wao.
Familia zatengana kwa siku kadhaa
Mkazi wa Dar es Salaam aliyejitambulisha kwa jina la Wema, ameeleza namna alivyoishi siku nne bila kuonana na familia yake, baada ya kupewa hifadhi Mbezi kwa Yusuph.
“Tulipofanikiwa kuvuka lile eneo, bosi wetu alisema hamshushi mtu njiani. Kwa hali ilivyokuwa, yeye na mkewe walituhifadhi kwao tangu jioni ya Oktoba 29 hadi tulipopata msaada jioni ya Novemba mosi,” amesema.
Maria Deogratius (si jina lake halisi) ameeleza namna alivyolazimika kumuachisha kunyonya mtoto wake mchanga.
“Vurugu zilipoanza sikuweza kufika kwangu Mbezi Malamba Mawili. Nilihifadhiwa siku nne kwa watu, baada ya kukwama njiani nikiwa natoka kazini. Nikalazimika kumwachisha mwanangu wa mwaka mmoja kunyonya,” amesema.
Natalia yeye alipotezana na baba yake kwa siku sita, tangu Oktoba 29 alipotoka kwenda kazini hadi Novemba 3.
“Tulisikia alipigwa risasi ya mguu akapelekwa hospitalini. Kuanzia hapo hatukuwahi kuwasiliana naye, simu yake ilikuwa ikiita na sasa haipatikani,” amesema kwa huzuni.
Dar hadi Kibaha ni ukaguzi
Mmoja wa waandishi wa makala hii, Imani Makongoro, ameeleza hali ilivyokuwa katika Barabara ya Morogoro kutoka Mbezi Mwisho hadi Kibaha.
Amesema tangu Oktoba 30 walizuiwa kupita njia hiyo kutokana na kutokuwa na gari binafsi, usafiri wa umma wala pikipiki iliyoruhusiwa.
“Hata nilipoomba msaada wa polisi bado ilishindikana, hadi jioni ya Novemba mosi ndipo tulipopata msaada wa ofisa wa jeshi aliyekuwa na gari binafsi.
“Pamoja na hilo, kutoka Mbezi hadi Kibaha kwa Mfipa tulikutana na vizuizi Kibamba, Kiluvya kwa Komba, Kiluvya Madukani, Mpakani, Njuweni, Picha ya Ndege, Kwa Mathias na Msikitini.
“Kote huko kulikuwa na polisi wa kutuliza ghasia na wanajeshi,” amesema.
Nauli, vyakula vyapanda
Vurugu hizo zimesababisha bei ya vyakula na nauli za bodaboda kupanda kati ya mara mbili hadi mara tano ya bei ya awali.
Baadhi ya bodaboda wachache waliendelea na kazi wakidai ugumu wa upatikanaji mafuta umechangia kupanda kwa nauli.
“Kwanza hatukuruhusiwa kuingia barabara kuu, tunapita njia za ndani. Pia mafuta yameadimika, tumeuziwa hadi mara tatu ya bei ya awali, hivyo nasi tukaongeza nauli. Mfano, sehemu ambayo ilikuwa nauli buku (Sh1,000), tulienda Sh4,000 hadi 5,000,” amesema mmoja wa bodaboda.
Mbali na nauli, kilo moja ya unga wa sembe ilipanda kutoka Sh1,300 hadi Sh2,000, na maduka mengine yaliuza hadi Sh2,500.
Mchele kilo moja ulifika hadi Sh4,000 katika baadhi ya maeneo kutoka Sh2,500, wakati unga wa ngano ulifika hadi Sh3,000 kwa kilo moja.
Licha ya bei kuwa juu, wateja katika maeneo mengi walilazimika kununua kwa kupanga foleni.
“Ni ngumu kupata bidhaa, huko tunakouziwa wamepandisha bei, hivyo ili nasi tupate faida,” amesema Nasra Hamed, mmoja wa wafanyabiashara wa nafaka.
Mtazamo wa kiuchumi
Mtaalamu wa Uchumi na Biashara, Oscar Mkude, amesema hali hii imeathiri kila mmoja, kwani hakuna aliyekuwa ameandaa mazingira ya kumpunguzia athari kama hali hii ingelitokea.
“Si wafanyabiashara pekee, bali watu wengi wamepata athari kwa sababu shughuli zimesimama moja kwa moja. Hata kufanya kazi nyumbani ilikuwa ngumu kwa sababu hakuna mtandao.
“Wengi walikuwa likizo isiyo rasmi, kwani kuna wanaohitaji watu ofisini. Wengi wameshindwa kuendelea na shughuli za kawaida, wameshindwa kufanya uuzalishaji, wamepoteza kipato, wengine wamepoteza kiasi cha pesa walichokuwa wakiingiza kila siku,” amesema.
Amesema hali hiyo inaweza kuwa mbaya hasa kwa wale wenye madeni, huku akiwataka wanaowadai kuwapatia kipindi cha msamaha kwani huenda wakashindwa kulipa kama walivyokubaliana awali.
Pia amesema ili kuzuia hali hii isitokee tena, ni vyema vyama kuangalia ni kwa nini nchi imefika hapo, kwani ni jambo lililotokea kwa muda mfupi lakini limeleta taharuki na uharibifu mkubwa wa miundombinu na biashara.
Amesema kitendo cha watu kuwa na likizo zisizo rasmi kimerudisha nyuma maendeleo ya watu, hivyo ni vyema kuwa na mshikamano wa kitaifa ili kutibu majeraha yaliyoachwa.
“Tunahitaji kuona wadau wote wanaohusika wanakaa katika meza moja. Si wote waliopo madarakani pekee, hata wale ambao hawakushiriki katika uchaguzi huu. Tuwe na maridhiano ili tuliponye taifa na tujenge uchumi kwenda mbele, kwani taifa bado lina watu wengi ambao kesho yao ina mashaka,” amesema Mkude.