Tarehe 13 Aban (4 Novemba) inafahamika katika kalenda ya Iran kama “Siku ya Taifa ya Kupambana na Uistikbari Duniani”.

Siku hii inasadifiana na kumbukumbu ya kutekwa “Pango la Ujasusi” la uliokuwa ubalozi wa Marekani hapa mjini Tehran mnamo mwaka 1979.

Tukio hili halikuwa ni jibu tu kwa Marekani kuendelea kuingilia masuala ya ndani ya Iran, bali pia ilikuwa ni hatua ya mabadiliko katika mwamko wa kisiasa wa taifa la Iran na nembo ya mshikamano wa kitaifa dhidi ya siasa za kupenda kujitanua za nchi za Magharibi.

Ubalozi wa Marekani mjini Tehran, ambao ulikuwa “Pango la Ujasusi” ulijulikana kama kituo cha kubuni na kutekeleza mipango ya kijasusi, kisiasa na kiusalama dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran. Nyaraka zilizopatikana ndani ya ubalozi huo zilifichua uingiliaji mkubwa wa Marekani katika masuala ya ndani ya Iran kuanzia zama za Pahlavi hadi baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Miongoni mwa mambo muhimu zaidi ya uingiliaji kati huu ilikuwa nafasi ya moja kwa moja ya Marekani katika mapinduzi ya Agosti 19, 1953, na uungaji mkono wake usio na masharti kwa utawala dhalimu.

Kufichuliwa kwa nyaraka hizi kulidhihirisha sura halisi ya sera za Marekani kwa watu wa Iran na walimwengu, na kulionyesha kwamba balozi zinaweza kuwa msingi wa ujasusi na njama dhidi ya mataifa.

Kutekwa ubalozi wa Marekani lilikuwa ni vuguvugu la hiari lililoibuka kutoka kwa jamii ya wanamapinduzi ya Iran. Kwa hatua hiyo, wanafunzi wanaofuata fikra za Imam Khomeini (RA) hawakuonyesha tu upinzani wao dhidi ya siasa za uingiliaji kati za Marekani, bali pia walifungua njia ya kuanzishwa kwa msamiati wa “chuki dhidi ya ubeberu” katika fasihii ya kisiasa ya mapinduzi.

Imamu Khamenei akihutubia hadhara ya wanachuo na wananchi

Akihutubia maelfu ya wanafunzi, wanachuo na familia za mashahidi wa Vita vya Siku 12 Jumatatu ya jana kwa mnasaba wa kukaribia tarehe 4 Novemba ya kuadhimisha “Siku ya Wanafunzi na Siku ya Taifa ya Kupambana na Uistikbari Duniani” ambayo inasadifiana na kumbukumbu ya kutekwa “Pango la Ujasusi” la uliokuwa ubalozi wa Marekani hapa mjini Tehran mnamo mwaka 1979 Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisisitiza kuwa, tukio hilo ni la kihistoria na linalobainisha utambulisho.

Ayatullah Sayyid Ali khamenei amesema kuwa, “mzozo uliopo kati ya Jamhuri ya Kiislamu na Marekani ni wa dhati halisi, na ni wa mgongano wa maslahi kati ya pande mbili. Ni ikiwa tu Marekani itakomesha kikamilifu uungaji mkono wake kwa utawala uliolaaniwa wa Kizayuni, ikaondoa kambi zake za kijeshi katika eneo, na kuacha uingiliaji wake, ndipo ombi la Marekani la ushirikiano na Iran litazingatiwa, na si sasa hivi au katika siku za karibuni, bali ni hapo baadaye”.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amekuelezea kutekwa kwa ubalozi wa Marekani mwaka 1979 kuwa ni “siku ya fahari na ushindi” na kielelezo cha utambulisho halisi wa serikali ya Marekani.

Amesema: “kutekwa kwa ubalozi wa Marekani kulifichua utambulisho halisi wa serikali ya Marekani na dhati halisi ya Mapinduzi ya Kiislamu”.

Ayatullah Khamenei ameeleza kwamba chimbuko la mivutano kati ya Marekani na Iran linarejea kwenye mapinduzi ya kijeshi ya 1953 yaliyompindua Waziri Mkuu Mohammad Mossadegh. Amesema, Marekani ilikula njama na Uingereza kumuangusha Mossadegh licha ya kujionyesha hadharani kuwa inamuunga mkono.

“Wamarekani walionyesha tabasamu kwa Mossadegh, lakini kisirisiri, na kwa kushirikiana na Waingereza, waliandaa mapinduzi ya kijeshi, wakaipindua serikali ya kitaifa, na kumrudisha Shah aliyekuwa anatoroka (nchi)”, ameeleza Kiongozi wa Mapinduzi.

Kwa hakika tarehe 13 Aban (Novemba 4) ni zaidi ya tukio la kihistoria, ni ishara ya mwamko wa kisiasa, kufichua sura halisi ya ubeberu wa kimataifa na umoja wa kitaifa dhidi ya uingiliaji wa kigeni. Siku hii ni ukumbusho wa ukweli kwamba, uhuru, utu na usalama wa taifa vitahifadhiwa tu kupitia kusimama kidete, ufahamu na umoja wa watu dhidi ya satwa na kujitanua.

Kwa kusoma tena tukio hili, kizazi kipya cha leo kinaweza kuendeleza njia ya muqawama, utambuzi, na kudumisha mamlaka ya kujitawa, na kufanya mambo kwa uangalifu na kuwa macho dhidi ya ushawishi na uingiliaji wowote wa kigeni.

Kutekwa Pango la Ujasusi (uliokuwa ubalozi wa Marekani mjini Tehran) kulikuwa ni jibu la kujihami dhidi ya njama kubwa ya kukkabiliana na harakati ya Kiislamu ya watu wa Iran. Hatua hii iliuonyesha ulimwengu utambulisho huru na wa kupinga ubeberu wa Mapinduzi ya Kiislamu; utambulisho ambao uliiwezesha Iran, katika vita vya Juni mwaka huu (2025) kukabiliana peke yake na kutegemea nguvu zake za ndani, sio tu dhidi ya utawala wa Kizayuni bali pia dhidi ya mfumo mzima wa ubeberu kwa muda wa siku 12, na kuzuia maadui kufikia malengo yao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *