
Dar es Salaam. Trauma ‘kiwewe’ haitokani na kuumizwa kimwili pekee, bali pia na kile unachoshuhudia.
“Kila nikisikia mlipuko wa tairi, moyo wangu hushtuka.” Kauli ya Amina Soud (26), Mkazi wa Buguruni mama wa watoto wawili, amesema tangu siku hiyo amekuwa akihisi hofu kubwa kila anaposikia mlio wa tairi au fataki.
“Nilikuwa sokoni siku hiyo. Ghafla nilisikia risasi, watu wakapiga kelele. Nilijificha chini ya meza. Tangu siku hiyo, kila sauti kubwa inanifanya nikimbie au nijifiche. Nilijua nimepona, kumbe akili yangu bado iko pale,” amesema.
Wakati risasi zinapiga, mabomu kulipuka na hofu kutanda, si waliojeruhiwa pekee wanaobeba maumivu hata waliokuwa mashuhuda hubeba alama za ndani ambazo hazionekani kwa macho.
Mara nyingi, mtu anaweza kuendelea na maisha akidhani amepona, kumbe ndani yake amebeba kiwewe (trauma) kinachoweza kuathiri afya ya akili na mwili kwa muda mrefu.
Wataalamu wa afya ya akili wanasema hali kama hii ni ya kawaida kwa watu waliopitia matukio ya kushtua kama hayo. Wengine hupata usingizi wa shida, ndoto mbaya, au kujiona kama wapo tena katikati ya tukio. Hii huitwa trauma ya baada ya tukio (Post-Traumatic Stress Disorder — PTSD).
Wamezitaja dalili kuwa umekumbwa na hali hiyo kisaikolojia na kihisia ni kuwa na kumbukumbu zinazorudia za tukio (flashbacks) wasiwasi, hasira, hofu, kukosa usingizi, kujitenga na watu au mazingira fulani.
Daktari wa Afya ya Akili kutoka Hospitali ya Kanda Mbeya, Dk Raymond Mgeni amesema janga ni tukio lolote linaloweza kutokea wakati usiotarajiwa na kuleta madhara ya kimwili, kiakili hadi kihisia.
Amesema matukio kama kusikiliza milio mikubwa ya vitu kama mabomu, kushuhudia tukio la kutisha husababisha msongo mkubwa wa mawazo hata baada ya tukio hilo kujitokeza.
“Hii husababisha wengine kuendelea kulikumbuka tukio, kushindwa kulala, kujawa na woga au wasiwasi au hata kuota ndoto za kutisha. Kisaikolojia matukio haya huweza kusababisha mtu kupata mahangaiko ya kiakili juu ya kukabiliana na tukio lilokwisha kutokea na hivyo huhitaji msaada ili hali isizidi kuwa mbaya zaidi,” ameshauri.
Dk Mgeni ametaja njia zinazoshauriwa kutumika kwa mtu ambaye kapitia janga na anapata hali ngumu kuvuka, moja ni kukubali kuwa janga kweli limetokea. Hii ni hatua ya awali kabisa ya kuruhusu kupona.
“Akili ikikataa kuwa hakukuwa na janga huzidi kuteseka zaidi. Pili ni epuka kuendelea kuwa katika mazingira ya kuchochea kumbukumbu za janga hasa baada ya janga kutokea siku za awali ili kuepusha hali mbaya zaidi ya mahangaiko katika akili,” amesema.
Pia, amesema ni muhimu kuzungumza kile unachopitia kwa kuandika na hili hupunguza maumivu na uchungu unaoweza kuwepo kwa wakati huo.
Pia, ni kuwa karibu na watu wengine wanaoweza kutoa mazingira ya kukutia moyo na matumaini juu ya hatua za kufuata baada ya mshtuko wa janga. Pia, kumuona mtaalamu wa afya ya akili endapo bado dalili za kushindwa kuvuka dhidi ya janga zikiendelea.
“Epuka matumizi ya vilevi kama pombe, bangi au sigara kama njia ya kusahau maumivu au uchungu. Hili litaongeza madhara mengine mapya kama uraibu wa vilevi kwa siku za baadae. Kaulimbiu ya mwaka huu inagusa umuhimu wa kufuata huduma za afya ya akili wakati wa dharura na majanga mapema ili kunusuru afya ya akili kuathiriwa,” amesema Dk Mgeni.
Daktari bingwa wa magonjwa ya akili Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Said Kuganda ameshauri kuwa ni muhimu waliopata trauma ya kisaikolojia wawe na watu wao wa karibu, ndugu wa kuwafariji na wa kuwasaidia, huku wakiepuka kukaa peke yao.
Amesema kwa kawaida mtu yeyote anaposikia sauti ya risasi au bomu lazima apate mshtuko, ni mwitikio wa kawaida na mara nyingi huendelea kupata mshtuko kwa kipindi cha mwezi mmoja.
Kwa mujibu wa Dk Kuganda mshtuko utaondoka kwa wengi iwapo mahitaji yao ya kila siku yatarudi ikiwemo vyakula, usafiri, ibada, kazi, shule na mahitaji mengine muhimu, humfanya mtu aliyeshtuka kurudi kuwa sawa.
“Mshtuko ni hali ya kawaida, kuwa na uhakika wa ile amani yako na hofu hupotea taratibu mwitikio wa namna ile hatuwezi kusema ni ugonjwa au maradhi ni mshtuko wa kawaida,” amesema na kuongeza;
“Kisaikolojia waliopitia majanga kama haya itachukua mwezi mzima kukaa sawa, mwingine ataogopa kutoka nje.”
Hata hivyo amesema ni muhimu kutoangalia picha mbaya iwe za kweli au za kutengenezwa na akili mnemba, hiyo itawasaidia watu kurudi sawa kwa haraka.
Amesema itahesabia kama mtu amepata trauma iwapo hali ya kushtuka na woga itaendelea kumzonga hata baada ya mwezi mmoja kupita, “Baada ya mwezi kupita wakawa bado hawako sawa, tutasema kuna tatizo watahitaji msaada wa tiba.”
Kwa mujibu wa Dk Kuganda walio katika hatari ya kupata trauma ni wale waliopoteza wapendwa wao, na kwamba wanahitaji faraja zaidi katika wakati huu na kwamba kundi hilo linaweza kukaa na hali ya huzuni hata miezi sita.
“Wanatakiwa kuwa na watu wa karibu wanaomfariji, huu msiba si wa kawaida tongeze kuwafariji ili wawe na matumaini na maombolezo,” amesema.
Madhara ya trauma isiyoshughulikiwa
Mtaalamu wa saikolojia tiba, Esther Hebron ameeleza jinsi trauma inavyojidhihirisha kimwili pale isiposhughulikiwa na kwamba tafiti nyingi zinaonyesha kuwa trauma isipotibiwa huathiri afya ya kimwili.
Amesema utafiti wa Adverse Childhood Experiences (ACE) uliofanywa na CDC na Kaiser Permanente ulionyesha uhusiano mkubwa kati ya matukio ya mshtuko utotoni na matatizo ya kiafya ukubwani.
Hebron amesema watu wenye alama za juu za ACE wana uwezekano mkubwa wa kupata magonjwa sugu kama shinikizo la damu, kisukari na magonjwa ya moyo.
“Trauma isiyoshughulikiwa hujidhihirisha kimwili kupitia maumivu ya kichwa, tumbo, au sehemu nyingine za mwili bila sababu za kiafya zinazojulikana. Pia huleta mabadiliko ya usingizi kama kukosa usingizi, kuamka mara kwa mara usiku au kulala kupita kiasi. Wengine hupata uchovu wa kudumu na kushuka kwa ari ya kufanya shughuli,” amesema.
Tafiti za American Psychological Association (APA) zinaonyesha kuwa watu waliopitia trauma wako kwenye hatari kubwa ya kupata wasiwasi, panic attacks, au PTSD, ambazo huambatana na dalili za kimwili kama maumivu ya kichwa na tumbo.
Hebron amesema watu wengi hukimbilia pombe au dawa za kulevya kama njia ya kupunguza maumivu ya kihisia, jambo linaloweza kusababisha utegemezi na matatizo zaidi.
“Ili kupona, ni muhimu kutafuta msaada wa kitaalamu kama ushauri nasaha, CBT au EMDR. Kuongea na watu wa karibu, kushiriki kwenye vikundi vya usaidizi, kufanya mazoezi, kulala vya kutosha, kula vizuri na kujihusisha na shughuli za kiroho au kuandika hisia binafsi husaidia mwili na akili kupona. Kupona kutokana na trauma ni mchakato unaohitaji muda, uvumilivu na kujitunza kwa makini,” amesema.