Ujerumani na Ghana zinataka kuimarisha mahusiano yao zaidi kwa kuendesha mashauriano ya kisiasa ya ngazi za juu, mara kwa mara, kujadili masuala yanayohusu maslahi ya pamoja.
Mpango huo umeelezwa na rais wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier ambaye yuko ziarani barani Afrika.
Kiongozi huyo wa Ujerumani ambaye aliwasili Jumapili mjini Accra, Ghana akitokea nchini Misri amefanya mazungumzo na mwenyeji wake rais John Mahama yaliyogusia masuala mbali mbali ikiwemo uwekezaji.
Steinmeier aliyeongozana na ujumbe wa wafanyabiashara kwenye ziara hiyo ameitaja Ghana kama nchi iliyoko kwenye nafasi nzuri kuliko mataifa mengine ya Afrika, kuvutia makampuni mengi.
“Nina furaha kutangaza kwamba leo pia tumefanikiwa kuleta habari njema ambazo zinasubiri kuidhinishwa na bunge la Ujerumani. Nchi yetu Ujerumani kwa mara nyingine itawekeza zaidi ya yuro milioni 65 katika mpango wa ushikiriano wa maendeleo”
Steinmeier alipokelewa kwa heshima za kijeshi na rais John Mahama ambaye pia kwa upande wake aliusifu urafiki uliopo baina ya Ghana na Ujerumani tangu nchi hiyo ya Afrika Magharibi ilipopata uhuru wake mnamo mwaka 1957.
Rais Mahama ameitaja ziara ya rais Steinmeier kuwa muhimu katika mahusiano ya mataifa hayo mawili akisema kwamba Ujerumani siku zote imekuwa mshirika wa kuaminika kwa Ghana.
” Rais Steinmeier na mimi tumefanya mazungumzo mazuri na ya uwazi kuhusu amani na usalama katika kanda ya Afrika Magharibi na hususan kuhusu kuongezeka kwa vitisho vya ugaidi,ghasia za makundi ya itikadi kali na ukosefu wa uthabiti wa kisiasa kwenye kanda ya Sahel . Nimemueleza rais kuhusu nafasi ya Kidiplomasia ya Ghana katika kujenga mdahalo,hali ya kuaminiana na kuimarisha ushirikiano miongoni mwa mataifa jirani ya kikanda.”
Rais wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier amelisifu bara la Afrika ambalo ni eneo la biashara huru lenye zaidi ya wakaazi bilioni 1.3, akisema linatowa fursa nzuri kwa Ujerumani na mataifa mengine.
Viongozi wa masuala ya kibiashara nchini Ujerumani wameitaja ziara ya Steinmeier nchini Ghana na Angola kama hatua muhimu ya kuimarisha uwepo wa kisiasa na kiuchumi kwa Ujerumani barani Afrika.