Wakati huu ripoti ya Umoja wa Mataifa ikionya kwamba uzalishaji wa kaboni duniani kote unaongezeka, rais wa Brazil Lula Inacio Da Silva ambaye nchi yake itakuwa mwenyeji wa mkutano wa COP30, anasema utakuwa ni mkutano wa kuambiana ukweli na kutoa suluhisho halisi.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Umoja wa Mataifa umesema licha ya miongo mitatu ya mazungumzo, nchi zitashindwa kudhibiti ongezeko la joto kwa nyuzi 1.5 kama ilivyoafikiwa chini ya Mkataba wa Paris muongo mmoja uliopita.
Aidha umoja huo umesema kwa kasi ya utoaji wa gesi chafu unaoendelea, ni wazi kiwango cha joto kitaongezeka kwa kati ya nyuzi 2.3 hadi 2.5 ikiwa hatua za haraka hazitachukuliwa.
Shirika la mazingira UNEP linasema itakuwa vigumu kurejea katika udhibiti wa nyuzi joto 1.5 ikiwa mataifa yatashindwa kutimiza ahadi walizotoa kukabiliana na athari za tabianchi.

Kuelekea mkutano wa COP30 utakaofanyika huko Belem, Brazil kuanzia Novemba 10 hadi 21, rais Lula da Silva anasema nchi Tajiri kushindwa kutimiza ahadi ilizotoa katika mikataba iliyopita, kunawakatisha tamaa raia duniani kote, sasa akiwataka viongozi watakaohudhuria kongamano hilo kuonesha utashi wa kisiasa.
Brazil inatarajiwa kupendekeza kuundwa kwa baraza jipya la mazingira la kimataifa linalohusishwa na Umoja wa Mataifa lenye mamlaka ya kufanya ziara na kufuatilia maendeleo ya ahadi za hali ya hewa.