Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS, imekanusha kama ya uongo na yenye hatari madai kwamba makundi yenye misimamo mikali katika eneo hilo yanawalenga watu wa dini fulani au yanafanya mauaji ya kimbari dhidi ya Wakristo.

Taarifa hii inatolewa baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kutishia kuchukua hatua za kijeshi nchini Nigeria kutokana na kile alichokiita “mauaji ya halaiki ya Wakristo.”

Kupitia taarifa iliyotolewa Jumanne, ECOWAS imesema madai kama hayo yanaweza kuongeza hali ya kutokuwa na usalama na kudhoofisha mshikamano wa kijamii katika eneo ambalo tayari linakabiliwa na vurugu za kigaidi.

“Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) inapenda kuwakumbusha washirika na jumuiya ya kimataifa kuhusu ongezeko la kiwango cha vurugu ambazo makundi ya kigaidi ya aina mbalimbali yamekuwa yakifanya katika baadhi ya nchi za eneo hili, zikiwemo Nigeria,” taarifa hiyo ilisema.

ECOWAS ilisisitiza kwamba mashambulizi ya kigaidi katika Afrika Magharibi yanalenga raia wasio na hatia bila kujali dini, kabila, au jinsia.

Trump alitangaza kwenye mitandao ya kijamii mwishoni mwa juma lililopita kwamba ameiamuru Wizara ya Vita ya Marekani (Pentagon) kuandaa mpango tarajiwa wa kutekeleza mashambulizi ya kijeshi “kukabiliana na mauaji makubwa ya Wakristo nchini Nigeria.”

Wakati huo huo, Waislamu na Wakristo wa Nigeria wamesisitiza kuishi pamoja kwa amani na maelewano na kusema kuwa vitisho vya Rais wa Marekani dhidi ya nchi hiyo havikubaliki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *