Liverpool, England. Liverpool imerudi katika kiwango chake baada ya kuichapa Real Madrid katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kwenye Uwanja wa Anfield usiku wa Novemba 4, 2025.
Mabingwa hao wa England chini ya kocha Arne Slot, walimaliza kipindi kigumu cha kupoteza mechi sita kati ya saba kwa ushindi dhidi ya Aston Villa, Jumamosi iliyopita na mwendelezo wa mafanikio uliendelea huku Real Madrid wakizidiwa kila idara.
Ushindi wa Liverpool ulikuwa wa kishindo zaidi ya matokeo yanavyoonyesha, huku Alexis Mac Allister akivunja ukimya katika kipindi cha pili, wakati Trent Alexander-Arnold, aliyekuwa beki wa zamani wa Liverpool, akitazama mchezo kutokea benchi huku timu yake mpya ikiwa imezidiwa.
Kipa wa Madrid, Thibaut Courtois, alifanya kazi kubwa kuzuia michomo kwa mashambulizi mfululizo, ikiwemo mikwaju minne kutoka kwa Dominik Szoboszlai na mpira wa kichwa wa Virgil van Dijk uliookolewa kwa ustadi wa hali ya juu.
Hata hivyo, Courtois hakuweza kuzuia bao la Liverpool, wakati Mac Allister alipopiga kichwa mpira wa adhabu uliopigwa na Szoboszlai katika dakika ya 61.
Alexander-Arnold aliingia uwanjani dakika kumi za mwisho za mchezo, huku akizomewa na mashabiki wa Liverpool waliowahi kumshangilia kipindi anaitumikia klabu hiyo.
Wachezaji nyota wa Madrid, Jude Bellingham na Kylian Mbappe, walizimwa kabisa, na hawakuweza kuizuia timu ya Slot kupata alama tatu muhimu ikiwa nyumbani.
Arsenal yaweka rekodi
Mikel Merino alifunga mabao mawili wakati Arsenal ikiibuka na ushindi mnono wa 0-3 dhidi ya Slavia Prague katika mechi iliyochezwa Fortuna Arena, jana Jumanne Novemba 4, 2025 na kuongeza mfululizo wao wa ushindi hadi mechi nane mfululizo katika mashindano yote.
Ushindi huo pia ulikuwa ni wa nane mfululizo bila kuruhusu bao, jambo lililoifanya kufikia rekodi ya klabu iliyowekwa mwaka 1903 katika misimu miwili tofauti.
Merino alianza kama mshambuliaji wa mwisho kuchukua nafasi ya Viktor Gyökeres aliyekuwa majeruhi, na kama alivyofanya msimu uliopita alipomrithi Kai Havertz, kiungo huyo alionyesha tena uwezo wake wa kucheza nafasi mbalimbali na kutoa mchango muhimu kwa Arsenal.
Kinda wa Arsenal, Max Dowman, ameweka rekodi mpya kuwa mchezaji mdogo zaidi kuwahi kucheza mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kuingia kama mchezaji wa akiba katika 72 kuchukua nafasi ya Leandro Trossard.
Akiwa na miaka 15 na siku 308, kinda huyo amevunja rekodi iliyowekwa na Youssoufa Moukoko, ambaye aliichezea Borussia Dortmund dhidi ya Zenit akiwa na miaka 16 na siku 18.
Diaz atupia mbili Bayern ikiifunga PSG
Mabao mawili ya Luis Díaz yameisaidia Bayern Munich iliyomaliza na wachezaji 10 kuendeleza mwanzo wao mzuri kwa kuwashinda mabingwa watetezi wa Ulaya, Paris Saint-Germain (PSG).
Timu hiyo ya Ujerumani imefikisha ushindi wa 16 mfululizo katika michuano yote, ikiwemo michezo minne ya ushindi katika Ligi ya Mabingwa, na inaongoza msimamo.
Díaz alikuwa na usiku wenye mchanganyiko wa matukio, akifunga mabao mawili yaliyoiweka Bayern kifua mbele kabla hajatolewa uwanjani kwa kadi nyekundu muda mfupi kabla ya mapumziko, kufuatia rafu ya nyuma kwa Achraf Hakimi ambayo ilimwacha beki huyo wa PSG akiwa na maumivu makali ya kifundo cha mguu, akatolewa uwanjani huku akilia.
Napol yabanwa
Napol imeshindwa kupata ushindi kwa mara ya pili mfululizo baada ya mabingwa hao wa Italia kulazimishwa matokeo ya suluhu nyumbani dhidi ya Eintracht Frankfurt kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, katika Uwanja wa Diego Armando Maradona.
Kikosi cha Antonio Conte kilikuwa kinatafuta kujirekebisha baada ya kichapo cha mabao 6–2 kutoka kwa PSV Eindhoven katika mchezo wa tatu wa makundi, lakini kilihangaika kutengeneza nafasi huku kikimkosa kiungo Kevin De Bruyne aliye majeruhi.
Spurs yagawa dozi
Mabao kutoka kwa Brennan Johnson na Wilson Odobert yaliwaweka Spurs kifua mbele kwa mabao mawili na kuonekana kama tayari wameimaliza mechi, kabla Johnson kuonyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja baada ya kuteleza na kumgusa Marcos Lopez kwenye kifundo cha mguu katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Tottenham Hotspur.
Lakini licha ya kucheza wakiwa pungufu ya mchezaji mmoja, Van de Ven alifunga moja ya mabao bora kabisa ya msimu. Alichukua mpira ndani ya nusu yao ya uwanja na kukimbia hadi mbele, akiwapita wachezaji wanne wa Copenhagen kabla ya kumalizia kwa ustadi ambao hata angekuwa mshambuliaji angejisifia kwa umaliziaji huo.
Spurs ilikuwa imezomewa na mashabiki wao mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Chelsea, lakini safari hii mashabiki walikuwa wamesimama wakishangilia kipindi chote cha pili huku Joao Palhinha akiongeza bao la nne.
Mambo yalikaribia kuwa mazuri zaidi kwa Tottenham ilipopewa penalti muda wa majeruhi, lakini Richarlison alikosa nafasi hiyo baada ya kupiga mpira na kugonga mwamba wa juu.
Ushindi huo unaifanya Tottenham kufikisha pointi nane baada ya mechi nne za Ligi ya Mabingwa, Tottenham wako nafasi ya saba katika msimamo wa UEFA ikiwa ni sehemu nzuri ya kumaliza ndani ya nane bora, jambo litakalowaruhusu kuruka hatua ya mchujo na moja kwa moja kuingia hatua ya 16 bora.