Muuguzi ahukumiwa kifungo cha maisha kwa kuuwa watu 10Muuguzi ahukumiwa kifungo cha maisha kwa kuuwa watu 10

Mahakama katika jiji la Aachen, magharibi mwa Ujerumani, imemhukumu muuguzi wa huduma za wagonjwa wa tiba ya maumivu kifungo cha maisha jela kwa kosa la kuua wagonjwa 10 na kujaribu kuua wengine 27 kwa kutumia sindano zenye dawa hatari.

Kwa mujibu wa uamuzi uliotolewa Jumatano, mahakama ilimkuta na hatia muuguzi huyo mwanaume mwenye umri wa miaka 44 kwa makosa yaliyofanyika kati ya Desemba 2023 na Mei 2024 katika hospitali moja mjini Würselen, karibu na Aachen.

Mahakama pia ilibaini kuwa makosa hayo yalihusisha “hatia kubwa”, jambo linalomaanisha hatakuwa na nafasi ya kuachiliwa mapema baada ya miaka 15 — jambo ambalo kwa kawaida linawezekana katika vifungo vya maisha. Jina la mtuhumiwa halikuwekwa hadharani.

Mwendesha mashtaka alimuelezea mshtakiwa kama mtu aliyekuwa “anaamuua kati ya maisha na kifo”, akiamua nani aishi na nani afe miongoni mwa wagonjwa aliowahudumia. Upande wa utetezi uliomba aachiwe huru, katika kesi iliyokuwa ikisikilizwa tangu Machi mwaka huu.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, muuguzi huyo aliwachoma wagonjwa — wengi wao wakiwa wazee — dozi kubwa za dawa za usingizi na za maumivu, kwa lengo la kupunguza kazi zake usiku.

Mahakama iliambiwa kuwa alikuwa na tatizo la kisaikolojia, hakuonyesha huruma, na hakuonyesha majuto yoyote wakati kesi ikiendelea.

Dawa alizotumia zilikuwa morphine na midazolam, dawa inayotumika pia katika utekelezaji wa adhabu ya kifo nchini Marekani.

Ukosefu wa Huruma watajwa

Waendesha mashtaka walimuelezea kama mtu aliyefanya kazi “bila ari wala motisha”, na kwamba alipokutana na wagonjwa waliokuwa na uhitaji mkubwa wa matunzo, alionyesha tu hasira na kutojali.

Mahakama ikiendelea kusikiliza shauri
Mahakama ikiendelea kusikiliza shauriPicha: Beatrice Jansen/photothek/IMAGO

Alimaliza mafunzo yake ya uuguzi mwaka 2007 na kufanya kazi kwa waajiri mbalimbali, ikiwemo katika mji wa Cologne. Tangu mwaka 2020, alikuwa akifanya kazi katika hospitali ya Würselen kabla ya kukamatwa majira ya kiangazi mwaka 2024.

Waendesha mashtaka waliiambia AFP kuwa miili ya wagonjwa imefukuliwa kwa ajili ya uchunguzi zaidi, na kwamba huenda atapandishwa tena kizimbani ikiwa watabainika waathirika wengine.

Itakumbukwa kuwa kesi hii imefananishwa na ile ya muuguzi Niels Hoegel, aliyehukumiwa kifungo cha maisha mwaka 2019 kwa kuua wagonjwa 85, na anayechukuliwa kama muuaji wa mfululizo mkubwa zaidi katika historia ya Ujerumani ya kisasa. Hoegel aliwaua wagonjwa kati ya mwaka 2000 na 2005 kwa sindano za sumu, kabla ya kukamatwa.

Wataalamu wa akili walisema alikuwa na tatizo kubwa la afya ya akili. Mnamo Julai 2024, mtaalamu mwingine wa tiba ya maumivu mwenye umri wa miaka 40, aliyejulikana na vyombo vya habari kama Johannes M., alianza kusikilizwa kesi yake jijini Berlin, akikabiliwa na tuhuma za kuwaua wagonjwa 15 kwa sindano zenye sumu kati ya mwaka 2021 na 2024.

Katika angalau kesi tano, anadaiwa kuchoma moto nyumba za waathirika wake ili kuficha ushahidi wa uhalifu wake.

Daktari mstaafu wa Ujerumani anayesaidia wakimbizi Uganda

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *