Sudan, ambayo kwa sasa imetumbukia katika kinamasi cha vita vya wenyewe kwa wenyewe, ni nchi yenye nguvu na uwezo mwingi.

Kwa miaka mingi, ardhi hii imekuwa katika mapambano ya mara kwa mara kati ya utambulisho wake halisi wa Kiafrika-Kiislamu na mfumo wa ubeberu wa kimataifa.

Kabla ya Sudan Kusini kujitenga, Sudan ilikuwa nchi kubwa zaidi ya Kiarabu na Kiislamu barani Afrika na kuwa miongoni mwa nchi kumi kwa ukubwa duniani. Kupakana na Bahari Nyekundu, kuwa kwake karibu na nchi nane muhimu katika bara hilo, na Mto Nile kupitia humo kumeifanya Sudan kuwa mojawapo ya maeneo nyeti zaidi ya kisiasa ya kijiografia duniani.

Licha ya uwezo wake mkubwa wa kiuchumi na kiutamaduni, kuanzia rasilimali nyingi za madini, mashamba yenye rutuba, na nguvukazi kijana hadi eneo lake la kimkakati lisilo na kifani, Sudan imeshuhudia zaidi ya mapinduzi 20 ya kijeshi, vita viwili vikuu vya wenyewe kwa wenyewe, na mamia ya maelfu ya vifo na kufurushwa watu tangu uhuru wake mwaka 1956.

Filihali Sudan imo katika lindi la vita vya wenyewe kwa wenyewe vya uchu wa madaraka kati ya Jeshi la Sudan (SAF) linaloongozwa na Abdul-Fattal al-Burhan na Kikosi cha Usaidizi wa Haraka (RSF), chini ya uongozi wa Hamdan Dagalo ambavyo vimesababisha hasara kubwa za kibinadamu na hasara za kifedha na mali kwa nchi hii kubwa ya Kiafrika.

Hebu na tuangalie kwa ufupi nukta za nguvu za Sudan katika nyanja mbalimbali:

Kijiografia Sudan iko kaskazini mashariki mwa bara la Afrika. Ilikuwa katika orodha ya nchi kumi kwa ukubwa duniani kabla ya kujitenga Sudan Kusini. Sudan bado ni nchi kubwa yenye eneo la kilomita za mraba 1,886,000. Mandhari ya Sudan ni tambarare kubwa, yenye milima na nyanda za juu kusini na mbali zaidi magharibi. Sudan iko katika eneo la kitropiki la Afrika.

Mto Nile Nyeupe na Nile Buluu ni uhai wa Sudan na kabla ya kitu kingine chochote, zimewezesha ustaarabu wake, maisha ya kiuchumi na kilimo. Sehemu ya kaskazini ya nchi kwa kiasi kikubwa ni jangwa, lakini mikoa ya kati na kusini ina ardhi yenye rutuba ambapo kilimo cha pamba na nafaka kina mizizi ya kihistoria.

Kwa upande wa hali ya hewa, Sudan ni mojawapo ya maeneo yenye joto kali zaidi duniani; lakini joto hili hili, pamoja na udongo wenye rutuba na maji ya Nile, yameifanya kuwa mojawapo ya ardhi yenye rutuba zaidi katika bara la Afrika.

–   Bahari Nyekundu, kwenye mpaka wa mashariki wa Sudan, ni njia muhimu kwa biashara ya kimataifa. Udhibiti au ushawishi juu ya pwani ya Sudan kwenye bahari hii unamaanisha ufuatiliaji wa njia za meli kati ya Asia, Mashariki ya Kati na Ulaya. Umuhimu huu wa kimkakati daima umeifanya Sudan kuwa shabaha ya mataifa makubwa, hasa baada ya migogoro ya kikanda na maendeleo ya bandari pinzani.

Mafuta ni mojawapo ya maliasili muhimu zaidi ya Sudan, lakini sekta hiyo inakabiliwa na changamoto kubwa. Uchimbaji wa mafuta nchini Sudan ulianza miaka ya 1970 na kupanuka katika miaka ya 1990 kwa kushirikisha makampuni ya kigeni.

Kujitenga Sudan Kusini na Sudan lilikuwa pigo kubwa zaidi kwa umoja na uchumi wa nchi hiyo. Visima vingi vya mafuta vilikuwa katika mikoa ya kusini, na kutokana na tangazo la uhuru la Juba, Khartoum ilipoteza chanzo chake kikuu cha mapato. Kabla ya kujitenga Sudan Kusini mwaka 2011, nchi hiyo ilizalisha takriban mapipa 500,000 kwa siku, lakini baada ya hapo, ilipoteza takriban asilimia 75 ya rasilimali zake za mafuta.

Katika miaka ya hivi karibuni, uzalishaji wa mafuta umeshuka na kufikia mapipa 30,000 hadi 60,000 kwa siku. Vita vya wenyewe kwa wenyewe na uharibifu wa miundombinu, ikiwa ni pamoja na mitambo ya kusafisha mafuta na mabomba, vimeipeleka sekta ya mafuta kwenye ukingo wa kuanguka na kusambaratika. Kabla ya 2011, mafuta yalitoa takriban nusu ya mapato ya serikali.

Salva Kiir Rais wa Sudan Kusini

Baada ya Sudan Kusini kujitenga, Sudan ililazimika kutegemea zaidi vyanzo vingine vya mapato, hasa madini ya dhahabu na kodi kubwa katika kilimo. Hali ya uchumi nchini Sudan imekuwa ikizidi kuzorota tangu Sudan Kusini ilipojinyakulia uhuru wake, na mapato ya mafuta nchini humo yameharibiwa vibaya na hivyo kupelekea serikali ya Sudan kuamua kutekeleza sera za kubana matumizi ili kudhibiti hali ya uchumi.

–    Sudan ni mojawapo ya nchi tajiri zaidi barani Afrika katika masuala ya rasilimali za madini, na migodi yake ina nafasi muhimu katika uchumi wa nchi hiyo. Sudan ina rasilimali nyingi za madini kutokana na utofauti wake wa kijiolojia. Madini muhimu zaidi nchini ni dhahabu, ambayo imekuwa ikichimbwa tangu zamani katika mikoa ya kaskazini kama vile Wadi Halfa hadi Atbara.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *