Kikao cha kwanza cha Baraza la Wawakilishi kilianza kwa kumchagua Zubeir Ali Maulid kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa Spika. Mwanasiasa huyo alikuwa anashikilia wadhifa huo wakati Baraza lililovunjwa mapema mwaka huu kupisha uchaguzi mkuu. Kati ya wajumbe 68 wa Baraza waliokuwepo wakati wa uchaguzi wa Spika, wajumbe 54 sawa na asilimia 94.6 walimpigia kura Zubeir, huku wagombea wawili kutoka vyama nyengine wakipata kura chache, kati ya tatu na sifuri.
Baada ya Spika Zubeir kula kiapo mbele ya Katibu wa Baraza hilo, Raya Issa Mselem, aliketi rasmi kuanza kazi kwa kuwaapisha wajumbe wapya wa Baraza la Wawakilishi, wakiwemo wachache kutoka chama cha ACT-Wazalendo ambacho kimeshinda majimbo kumi pekee ya kisiwa cha Pemba kati ya majimbo 50 ya visiwa vyote viwili vinavyounda eneo la Zanzibar.
Viapo “Mimi Nassra Nassor Omar naapa kwamba nitakuwa muaminifu kwa Zanzibar katika kazi zangu za uwakilishi na nitaitumikia kwa moyo wangu wote na kwamba nitaiihifadhi, nitailinda na nitaitetea kwa dhati katiba ya Zanzibar nakuomba Mwenyeenzi Mungu unisaidieā
ACT Wazalendo inatafakari iwapo ijiunge na serikali au la
Wajumbe wapya wa Baraza la Wawakilishi, wanaendelea kujisajili huku Naibu Spika anatarajiwa kupatikana kabla ya Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, kuhutubia na kulifungua rasmi Baraza la Kumi na Moja.
Awali ikulu ya Zanzibar ilitoa taarifa kuwa Rais Hussein Mwinyi amemteua Hemed Suleiman Abdulla kuwa Makamu wa Pili wa Rais. Hemed anaendelea na wadhifa huo alioshikilia wakati wa muhula wa kwanza wa rais Mwinyi. Atasubiri kuidhinishwa na Baraza la Wawakilishi kabla ya kuapishwa.
Chini ya katiba ya Zanzibar ilirekebishwa kufuatia kura ya maoni ya mwaka 2010, makamu wa pili wa rais ndiye mtendaji mkuu wa shughuli za kila siku za serikali. Pia mabadiliko hayo yaliunda nafasi ya makamu wa kwanza wa rais itakayoshukiliwa na mwanasiasa wa chama cha upinzani kilichoshika nafasi ya pili katika uchaguzi na kuridhia kujiunga kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.
Chama cha ACT Wazalendo kilichoshika nafasi ya pili bado kinatafakari iwapo kijiunge serikali hasa baada ya kusema uchaguzi uliomalizika ulikuwa na dosari. Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo aliyekuwa pia makamu wa kwanza wa rais , Othman Masoud amekamilisha awamu ya kwanza ya mikutano yake ya ndani kisiwani Unguja na sasa yupo kisiwani Pemba kwa ajili ya kukutana na viongozi wa chama na wanachama kujadili mustakabali wa chama na kuingia au kutokuingia kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNU).
Hata hivyo, kinachosubiriwa kwa hamu kwa sasa ni kuona iwapo kiongozi tarejea serikalini, pamoja na wizara ambazo Rais Mwinyi atawapatia wawakilishi kutoka upinzani.