Barcelona, Hispania. Klabu ya Barcelona inaonekana kuvutiwa na kiwango cha Marcus Rashford kiasi cha kutaka kumsajili moja kwa moja mwishoni mwa msimu huu, lakini mchezaji huyo wa Manchester United atalazimika kupunguza mshahara wake ili dili hilo likamilike.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka vyombo vya habari vya Ulaya, Rashford alijiunga na Barcelona kwa mkopo msimu huu wa kiangazi, huku kukiwa na kipengele cha kununuliwa moja kwa moja kwa pauni milioni 28 mwishoni mwa msimu.

Akiwa chini ya kocha Hansi Flick, mshambuliaji huyo wa England amekuwa moto wa kuotea mbali akifunga mabao sita na kutoa asisti saba katika mechi 14 pekee, na kupigiwa makofi ya shukrani (standing ovation) kutoka kwa mashabiki wa Barca baada ya kufunga kwenye ushindi wa 3-1 dhidi ya Elche mwishoni mwa wiki.

Barca wanamtaka lakini mshahara ni kikwazo

Mtaalamu wa soka la Ulaya, Andy Brassell, amesema kwenye podcast ya Trans Euro Express kuwa Barcelona wanataka kumbakisha Rashford kwa mkataba wa kudumu, lakini lazima akubali kukatwa mshahara tena.

“Wana mpango wa kumfanya kuwa mchezaji wao rasmi, si tu kuongeza mkopo mwingine. Amekuwa bora sana, na Hansi Flick amefurahishwa naye kabisa,” amesema Brassell.

“Rashford amejibeba vizuri, hasa kipindi hiki ambacho Raphinha amekuwa majeruhi. Anaelewana vizuri na vijana kama Lamine Yamal na Fermín López, na Barcelona wanaonekana hatari zaidi akiwa uwanjani.”

Bajeti finyu yabana mipango

Hata hivyo, changamoto kubwa kwa Barca ni hali yao ya kifedha. Klabu hiyo bado inakabiliwa na vizuizi vya matumizi vya La Liga, na italazimika kutumia ujanja wa kugawanya gharama za usajili kwa muda mrefu wa mkataba ili kufanikisha dili hilo.

“Barcelona hawana pesa nyingi, lakini wanaweza kueneza malipo hayo kwa miaka kadhaa,” Brassell aliongeza.

“Mpango ni kumpa Rashford mkataba mrefu zaidi, lakini kwa mshahara uleule wa sasa ambao tayari ni mdogo ukilinganisha na alivyokuwa akilipwa Manchester United.”

Rashford apata utulivu Hispania

Kwa upande wake, Rashford amewahi kusema anafurahia maisha yake nchini Hispania, akidai kuwa kuchezea Barcelona kumempa nafasi ya kutulia na kuzingatia mpira, bila shinikizo kubwa alilopata akiwa England.

Uhusiano wake mzuri na Hansi Flick, pamoja na nafasi anayopata katika kikosi cha kwanza, vinatajwa kuwa sababu kubwa zinazomfanya kutaka kubaki Camp Nou.

Kwa sasa, Barcelona wanaendelea kutathmini hali yao ya kifedha kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho, lakini dalili zinaonyesha wazi wanamtaka Rashford, ila kwa masharti yao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *