Ili kushughulikia changamoto hiyo, shirika moja nchini Kenya limeamua kutumia mchezo wa kandanda kama chombo cha kuleta mabadiliko katika jamii. Lengo kuu la kampeni hii ni kuwahamasisha vijana kutumia fursa zilizoko kupitia michezo kujiajiri, kubuni kazi, na hivyo kujikimu kimaisha.

“Tulikaa chini tukajiuliza, ni vipi tunaweza kutumia kandanda kuwaleta vijana pamoja ili kuwasaidia kupata au kuunda ajira zao wenyewe? Hapo ndipo wazo la kampeni hii lilipozaliwa,” anasema Bwana Omondi Peter, Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Shirika la Global Youth Forum linalojihusisha na utokomezaji wa umaskini barani Afrika kuanzia Kenya kwa kutumia michezo mbalimbali hususani mpira wa miguu.

Ni nini mustakabali wa kampeni hii

Kampeni hiyo, inayotarajiwa kufanyika mapema mwaka 2026, italeta pamoja timu 34 kutoka kaunti 17 nchini Kenya. Kila timu itawakilisha lengo moja la maendeleo endelevu, kulingana na eneo au ajenda wanayoipigia debe.

Mbali na kuwahamasisha vijana kuhusu SDGs, mashindano hayo pia yanawapa nafasi ya kuonyesha vipaji vyao na kujifunza ujuzi wa ujasiriamali.

Peter Omondi, Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Global Youth Forum linalounganisha vijana Kenya, akiwa na vijana wachezaji wa mpira wa miguu.

Global Youth Forum

Ushirikiano na Umoja wa Mataifa

Uhusiano wa kampeni hii na Umoja wa Mataifa ni wa karibu. Mnamo mwaka 2024, Umoja wa Mataifa uliteua tarehe 25 Mei kuwa Siku ya Kandanda Duniani, na mwaka 2022 ulizindua mpango maalum uitwao Football for the Goals. Mpango huo unaleta pamoja mashirika na taasisi zinazotumia kandanda kuendeleza malengo ya maendeleo endelevu.

Shirika hili nchini Kenya ni miongoni mwa wadau walioteuliwa kuandaa mashindano hayo kupitia mpango wa Football for the Goals Inaugural Tournament mwaka 2023, yakihusisha timu 16 kutoka kaunti mbalimbali nchini.

Vijana wachezaji wa soka ambao ni wanachama wa Global Youth Forum, shirika linalounganisha vijana wa Kenya kupitia michezo.

Global Youth Forum/Peter Omondi

Mambo yaliyozingatiwa

Tangu wakati huo, wameandaa mashindano matatu ya aina hiyo, kwa ushirikiano wa karibu na Umoja wa Mataifa.

“Umoja wa Mataifa umetusaidia sana katika maeneo matatu muhimu,” amesema mwakilishi wa shirika.

“Kwanza, wametusaidia kuhamasisha vijana mashinani kuhusu umuhimu wa SDGs. Pili, wametusaidia kupata wadhamini kusaidia vijana hawa kushiriki bila vikwazo vya kifedha. Tatu, wametupatia majukwaa ya mafunzo ambapo tumeshirikisha mashirika mengine mbinu tunazotumia kuandaa michezo inayochochea maendeleo endelevu.”

Kupitia juhudi hizi, shirika hilo linaendeleza kaulimbiu ya Umoja wa Mataifa ya “Kutoacha yeyote nyuma” na kuimarisha ushirikiano kuelekea kutimiza Ajenda ya Maendeleo Endelevu ya 2030.

Peter Omondi (kati), Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Global Youth Forum linalounganisha vijana Kenya, akiwa na vijana wachezaji wa mpira wa miguu.

Global Youth Forum/Peter Omondi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *