
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameonya kuwa kikosi chochote cha kurejesha uthabiti na utulivu kitakachopelekwa Ukanda wa Ghaza lazima kiwe na “uhalali kamili wa kimataifa” ili kuwasaidia Wapalestina wa eneo hilo.
Akizungumza katika mahojiano na televisheni ya Al Jazeera, katika Mkutano wa Pili wa Dunia wa Maendeleo ya Jamii, Guterres amesema, makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa baada ya “mateso na njaa kali” iliyokuwa imelikumba eneo hilo lililozingirwa na kushambuliwa kwa makombora, yameendelea kuwa tete na yanahitaji dhamana na hakikisho la kimataifa.
“Ni muhimu kikosi kinachoundwa kiwe na uhalali kamili wa kimataifa ili kukabiliana na pande zote na kuamiliana na jamii ya watu wa Ghaza”, ameeleza Katibu Mkuu wa UN.
Kikosi cha kimataifa kilichopendekezwa kwa ajili ya Ghaza ni sehemu ya mpango wa amani wa Ghaza wenye vipengee 20 uliotangazwa na Rais wa Marekani Donald Trump.
Hata hivyo kungali kuna utata kwamba ni mataifa gani yatakayounda kikosi hicho.
Licha ya kuwepo ukosoaji, Guterres amesema agizo kutoka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) linasalia kuwa “chanzo cha uhalali” kwa kikosi chochote cha kurejesha utulivu, akionya kwamba bila hilo, hatari ya kuibuka mzozo mpya ingali ya kiwango cha juu.
Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ameipongeza pia Marekani kwa kuifanya Israel ikubali kufikia makubaliano ya sasa ya usitishaji mapigano.
“Serikali ya Israel ilikuwa na nia nyingine … ambayo ilikuwa ni kuendesha vita hadi mwisho, lakini Wamarekani, kwa wakati fulani, walielewa kwamba hali ilipofikia inatosha”, amebainisha Guterres.
Kwa mujibu wa maafisa wa Ghaza, utawala wa kizayuni wa Israel umekiuka makubaliano hayo zaidi ya mara 80, na kuwaua mamia ya Wapalestina katika wiki nne zilizopita.
Mbali na hayo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameonya kuwa, msaada unaoingia Ukanda wa Ghaza kwa sasa ungali ni wa kiwango cha chini sana kulinganisha na kinachohitajika…/