
Ripoti hiyo, yenye kichwa, “kuchochea suluhisho kwa upatikanaji sawa duniani na ufadhili endelevu wa chanjo mpya za kifua kikuu kwa watu wazima na vijana,” imetoa uchambuzi wa kwanza wa aina yake kuhusu vikwazo vinavyotarajiwa, vizuizi, na mienendo ya soko ambayo inaweza kuathiri upatikanaji wa wakati, usawa, na endelevu wa chanjo mpya za TB.
“Chanjo mpya za TB zina uwezo wa kuokoa maisha ya mamilioni ya watu kwa haraka na kubadilisha mwelekeo wa janga hili, kwa kutumia nguvu ya sayansi, ushirikiano na fedha, tunaweza kufanikisha maono yetu ya pamoja ya kutokomeza kifua kikuu.” amesema Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu wa WHO.
Mahitaji ya chanjo mpya za kifua kikuu (TB) yatakuwa makubwa kuliko upatikanaji wake katika miaka ya mwanzo
Licha ya athari kubwa za kifua kikuu (TB) duniani, hakuna chanjo mpya iliyoidhinishwa kwa zaidi ya karne moja. Chanjo ya( Bacille Calmette-Guérin (BCG), ambayo imekuwa sehemu ya ratiba ya chanjo za utotoni katika nchi nyingi, hutoa ulinzi dhidi ya madhara makubwa zaidi ya TB kwa watoto wachanga na wachanga wadogo, lakini hutoa ulinzi mdogo na usiotabirika dhidi ya TB ya mapafu kwa vijana balehe na watu wazima.
Hata hivyo, kufikia Septemba 2025, angalau chanjo 16 mpya za TB zilikuwa katika hatua ya maendeleo ya majaribio ya kitabibu, zikiwemo 6 zikiwa katika awamu ya tatu (phase III trials).
Wakati utafiti na maendeleo ya chanjo haya yanapoongezeka kasi, na nchi nyingi zenye mzigo mkubwa wa TB zikianza kujiandaa kwa uzinduzi wa chanjo hizo, upatikanaji wa chanjo na ufadhili bado ni changamoto kubwa. Vivyo hivyo, wazalishaji wanakabiliwa na hali ya kutokuwa na uhakika kuhusu mahitaji ya nchi na upatikanaji wa fedha. Wazalishaji bado hawajatoa mikakati madhubuti ya upatikanaji, na uzalishaji wa kikanda wa chanjo haujapangwa kikamilifu katika kila eneo lenye mzigo mkubwa kwa chanjo zinazokaribia kukamilika.
Matokeo ya ripoti hii mpya yanaonesha kuwa mahitaji ya kimataifa ya chanjo za TB yatakuwa makubwa kuliko upatikanaji wake katika miaka ya mwanzo muhimu. Inakadiriwa kuwa mahitaji ya dunia yatazidi dozi bilioni 3 kati ya mwaka 2030 na 2040, huku nchi zenye mzigo mkubwa zikiongoza katika mahitaji hayo. Hata hivyo, makadirio ya upatikanaji yanaonyesha pengo katika miaka ya awali baada ya chanjo kusajiliwa, jambo linaloweza kusababisha ucheleweshaji wa upatikanaji na kupunguza athari chanya za kiafya kwa umma.
Gharama za ununuzi pekee zinakadiriwa kufikia kati ya dola za Kimarekani bilioni 5 hadi 8 katika kipindi cha miaka 2030–2040. Kiasi hiki hakijumuishi gharama za usambazaji wa chanjo wala gharama za kuimarisha mifumo ya afya kwa ajili ya utangulizi na utekelezaji wa chanjo hizo.
Kwa sasa, hakuna fedha maalum zilizotengwa kwa ajili ya chanjo mpya za TB, na nchi pamoja na wafadhili wanakabiliwa na maamuzi magumu ya kugawa rasilimali kati ya kuwekeza katika chanjo hizi mpya, juhudi nyingine za chanjo, hatua za sasa za kupambana na TB, na vipaumbele vingine vya afya wanapoanza kupanga mikakati ya ufadhili.
Suluhisho za kuhakikisha upatikanaji sawa wa chanjo mpya za kifua kikuu (TB)
Kulingana na vikwazo vilivyobainishwa katika uchambuzi wa mazingira, ripoti hii imeeleza suluhisho sita za kushinda changamoto katika kuhakikisha upatikanaji sawa wa chanjo mpya za TB:
1. Kutumia vyombo vya kimataifa vya kifedha na vya uundaji wa soko kama vile ahadi za soko za mapema na dhamana uhakika wa kiasi (volume guarantees) ili kuwahamasisha wazalishaji kuongeza uwezo wa uzalishaji na kujadiliana bei nafuu zaidi.
2. Kuzalisha ushahidi wa mapema katika ngazi ya nchi, kama vile utabiri wa mahitaji, uchambuzi wa ufanisi wa gharama, na tafiti za athari kwa bajeti, ambavyo vinaweza kuongoza maamuzi ya kitaifa kuhusu kupitishwa kwa chanjo;
3. Kufafanua ahadi za ufadhili wa ndani na ule wa wafadhili wa kimataifa, ili kubaini mapungufu na kuhamasisha rasilimali;
4. Kuweka jukwaa la uratibu kwa wadau wa usambazaji na mahitaji ili kusawazisha juhudi likiwa na ramani za pamoja za utekelezaji na mazungumzo ya mara kwa mara yatakayosaidia kulandanisha muda kati ya uzalishaji, ufadhili, na upatikanaji wa nchi.
5. Kushirikiana taarifa muhimu kuhusu upatikanaji wa bidhaa ambazo ni muhimu kwa upatikanaji sawa na zisizo za kibiashara, ili kusaidia mipango ya nchi na kujenga uaminifu kupitia uwazi wa soko na
6. Kuhamasisha uhamisho wa teknolojia na utoaji wa leseni kwa angalau mtengenezaji mmoja katika kila eneo lenye mzigo mkubwa, ili kuimarisha usalama wa usambazaji wa kikanda, umiliki wa ndani, na kukubalika kwa chanjo.
Uigaji wa modeli unaonesha kuwa, endapo chanjo itapitishwa na kusambazwa haraka, katika kipindi cha miaka 25, chanjo yenye ufanisi wa asilimia 50 katika kuzuia TB kwa vijana balehe na watu wazima inaweza kuzuia hadi visa milioni 76 vya TB, vifo milioni 8.5, mizunguko milioni 42 ya matumizi ya antibiotiki, na kuokoa hadi dola za Kimarekani bilioni 42 ambazo vinginevyo zingetumika na kaya zilizoathiriwa na TB.
Maendeleo na utekelezaji wa mikakati ya ufadhili na upatikanaji na nchi ni hatua muhimu katika mpango wa maandalizi na kuhakikisha upatikanaji sawa wa chanjo mpya za TB pindi zitakapopatikana.
Kwa uongozi thabiti wa kimataifa na ushirikiano, WHO itashirikiana na wadau wote kusukuma mbele utekelezaji wa suluhisho hizi kupitia Kikundi Kazi cha Fedha na Upatikanaji.
WHO inakaribisha uongozi unaoendelea kutoka kwa wanachama wa Kikundi Kazi katika juhudi hii ya kimataifa, ikiwemo kuweka ajenda ya hatua na mipango inayofuata.