Taarifa kutoka Kabul nchini Afghanistan na Vienna nchini Austria imeeleza kuwa kwa mujibu wa utafiti huo, eneo lililotumika kulima afyuni mwaka huu linakadiriwa kufikia hekta 10,200, likiwa ni punguzo la asilimia 20 ikilinganishwa na hekta 12,800 zilizoripotiwa mwaka 2024.

Takwimu hizo ni sehemu ndogo sana ya viwango vya kabla ya kilimo hicho kupigwa marufuku mwaka 2022, ambapo takribani hekta 232,000 zilikuwa zikilimwa nchi nzima.

Mapato ya wakulima yashuka

Kupungua kwa kilimo kumekwenda sambamba na kuporomoka kwa uzalishaji wa afyuni kwa asilimia 32, hadi tani 296 pekee mwaka 2025.

Mapato ya wakulima yameshuka kwa karibu nusu, kutoka dola milioni 260 mwaka jana hadi dola milioni 134 mwaka huu.

Shamba la afyuni katika jimbo la Kapisa nchini Afghanistan (Kutoka maktaba)

Shamba la afyuni katika jimbo la Kapisa nchini Afghanistan (Kutoka maktaba)

Mwakilishi wa Kanda wa UNODC katika nchi za Afghanistan, Asia ya Kati, Iran na Pakistan Oliver Stolpe amesema “Njia ya Afghanistan kupambana na kilimo haramu inahitaji uwekezaji wa muda mrefu na wa pamoja kupitia ushirikiano wa kimataifa. Ni muhimu kuwawezesha wakulima kupata vyanzo mbadala vya kipato, kuimarisha juhudi za kutokomeza mimea haramu na kudhibiti biashara ya dawa za kulevya,”

Baada ya marufuku ya uzalishaji wa zao hilo wakulima wengi wamegeukia kilimo cha nafaka na mazao mengine, lakini ukame na mvua chache vimesababisha zaidi ya asilimia 40 ya mashamba kubaki bila kulimwa.

Wakati huo huo, takribani watu milioni nne waliorejea Afghanistan kutoka nchi jirani wameongeza ushindani wa ajira na rasilimali, huku kupungua kwa misaada ya kibinadamu kukiibua hofu kwamba baadhi ya wakulima wanaweza kurudi kwenye kilimo cha afyuni kama njia ya kujipatia kipato.

Juhudi za kimataifa kupamana na uzalishaji wa afyuni

Naibu Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan na Kaimu Mkuu wa UNAMA, amesema “Tatizo la dawa za kulevya la Afghanistan si la ndani pekee. Linahusisha wahusika wa ndani na wa kimataifa, hivyo linahitaji ushirikiano mpana katika kudhibiti usambazaji, mahitaji na biashara ya dawa hizo.”

Ripoti hiyo ya UNODC inaonesha kuwa bei ya afyuni kavu imeshuka kwa asilimia 27, kutoka dola 780 mwaka 2024 hadi dola 570 mwaka huu, ingawa bado ni zaidi ya mara tano ya bei kabla ya marufuku. Mabadiliko haya ya bei na uzalishaji yanaashiria mabadiliko katika masoko na njia za usafirishaji, huku ikihofiwa kwamba nchi nyingine zinaweza kuanza kilimo haramu ili kujaza pengo hilo.

Ripoti hiyo inaongeza kuwa uzalishaji na biashara ya dawa haramu, hususan methamphetamine, unaendelea kuongezeka tangu marufuku ya afyuni.

Kukamatwa kwa dawa hizo kumeongezeka kwa asilimia 50 mwishoni mwa 2024 ikilinganishwa na kipindi kama hicho cha mwaka uliopita.

UNODC inasisitiza kuwa mikakati ya kupambana na dawa za kulevya sasa lazima ijumuishe pia dawa bandia, ambazo ni rahisi kuzalisha na kugundua kwa kiwango kidogo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *