Misitu ya kitropiki, ambayo ni muhimu katika mapambano dhidi ya uharibifu wa tabianchi, inaendelea kutoweka kwa kasi ya kutisha. Ni kwa mantiki hiyo leo Alhamisi, katika mkutano wa viongozi wa dunia unaofanyika Belém, lango kuu la kuingia katika msitu wa Amazon nchini Brazil, taifa hilo limezindua mfuko mpya wa kuimarisha ulinzi wa hazina hiyo
Hatua hii inakuja kabla ya Mkutano wa 30 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP30, mkutano utakaoanza mjini humo Jumatatu hadi tarehe 21 Novemba.
Mfuko huo, unaojulikana kama Taasisi ya Kudumu ya Misitu ya Kitropiki (Tropical Forests Forever Facility), utazipa motisha nchi zitakazofanikiwa kusitisha ukataji miti hovyo. Katika kuongeza thamani ya misitu hai kuliko ardhi iliyokatwa miti, mfuko huo unaweza kuelekeza hadi dola bilioni 4 kwa mwaka kwa nchi takribani 74.
Misitu ya kitropiki ni muhimu kwa uthabiti wa tabianchi
“Misitu ya kitropiki hupuliza uhai katika sayari yetu. Hata hivyo, bado inashambuliwa bila huruma—inaonwa kama faida ya muda mfupi badala ya thamani ya muda mrefu,” amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, akisisitiza umuhimu wa haraka wakati wa uzinduzi huo.
Kupitia mfuko huo, nchi zitakazohifadhi misitu yao zitapokea dola 4 kwa eka kwa mwaka, kiwango kitakachorekebishwa kulingana na utendaji uliothibitishwa kwa kutumia ufuatiliaji wa setilaiti.
Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC FAO kwa ushirikiano na wadau wamefanya ufuatiliaji wa aina za miti kwenye misitu, ikiwa ni mara ya kwanza.
Jumla ya nchi 74 zina sifa ya kushiriki, zikiwa na zaidi ya eka bilioni moja za misitu ya kitropiki na ya chini ya kitropiki. Maeneo yenye kipaumbele ni pamoja na Amazon, Msitu wa Atlantiki, Bonde la mto Congo, eneo la mto Mekong, na kisiwa cha Borneo huko Kusini Mashariki mwa Asia.
“Taasisi ya Kudumu ya Misitu ya Kitropiki ni mfumo jasiri wa kufanya misitu iliyo hai kuwa na thamani zaidi kuliko ardhi iliyokatwa miti – ikilinganisha uhifadhi na fursa, na mshikamano na ustawi wa pamoja,” amesema Bwana Guterres, akiongeza kwamba “misitu ya kitropiki ni muhimu kwa uthabiti wa hali ya hewa.”
“Pamoja, tunaweza kuhakikisha misitu ya kitropiki inabaki milele—ikiwa kama nguzo hai za uthabiti wa hali ya hewa, bioanuwai, uimara, na amani,” amesisitiza.
Kuunga mkono jamii za wenyeji
Wakati wa Wiki ya Mjadala wa Ngazi ya Juu ya Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa MAtaifa, UNGA, mwezi Septemba, Rais wa Brazil, Lula da Silva, alitangaza uwekezaji wa kwanza katika mfuko huo—dola bilioni moja.
Akizungumza na Idhaa ya Umoja wa Mataifa wakati huo, Mkurugenzi Mtendaji wa COP30, Ana Toni, alithibitisha kuwa asilimia 20 ya malipo ya kila nchi yataelekezwa moja kwa moja kwa jamii za wenyeji, ikisisitiza umuhimu wa watu wa jamii ya asili na wale wengine wanaolinda misitu katika jamii zao na nje yake.
“Hii inaonesha dhamira ya serikali ya Brazil si tu ya kuhifadhi misitu, bali pia kuwazawadia wale wanaoilinda, hasa Watu wa Asili,” amesema.
Kujenga ushirikiano wa kimataifa
Uundaji wa mfuko huu ulianza katika COP28 huko Dubai, Falme za Kiarabu mwaka 2023 na kufikia kilele chake katika uzinduzi rasmi kwenye COP30.
Hadi sasa, mataifa matano yenye misitu ya kitropiki yamejiunga: Colombia, Ghana, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Indonesia, na Malaysia.
Nchi zinazotarajiwa kuwekeza ni pamoja na Ujerumani, Falme za Kiarabu, Ufaransa, Norway, na Uingereza—zikichangia katika mfumo wa uwekezaji wa pamoja ambapo gawio litashirikiwa kati ya wawekezaji na mataifa yenye misitu.
Kuhamasisha mabilioni kwa ajili ya misitu
Serikali za wawekezaji zinatarajiwa kuchangia dola bilioni 25 katika miaka ijayo, zikivutia zaidi ya dola bilioni 100 kutoka kwa sekta binafsi. Brazil inakadiria kuwa mfuko huo unaweza kuzalisha takriban dola bilioni 4 kila mwaka—karibu mara tatu ya ufadhili wa sasa wa gharama nafuu kwa ajili ya ulinzi wa misitu.
Hata hivyo, fedha za kimataifa kwa ajili ya misitu bado hazitoshi.
Kulingana na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP), uwekezaji wa kila mwaka lazima uongezeke kutoka dola bilioni 84 mwaka 2023 hadi bilioni 300 kufikia mwaka 2030 na bilioni 498 kufikia mwaka 2050, na kuacha upungufu wa dola bilioni 216 kila mwaka.
Umuhimu wake
Kwa kuunganisha malipo ya kifedha na uhifadhi wa misitu, Taasisi ya Kudumu ya Misitu ya Kitropiki inalenga kubadilisha juhudi za dunia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na upotevu wa bioanuwai.
Mpango huu pia unaashiria mwelekeo mpya wa fedha za haki, jumuishi na zenye utabiri, kuhakikisha msaada unawafikia wale wanaolinda misitu kwa mikono yao, mioyo yao, na urithi wao.
COP30 italeta pamoja viongozi wa dunia, wajadiliani, na wadau ili kuharakisha hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, ukiweka mkazo mwaka huu kwenye misitu ya kitropiki, fedha, na suluhisho zinazotokana na mazingira.