
Familia ya mwalimu huyo imethibitisha kupokea taarifa za kifo cha mpendwa wao kutoka kwa rafiki yake mjini Dar es Salaam.
John Okoth Ogutu, mwalimu raia wa Kenya aliyekuwa akiishi Tanzania kwa miaka kumi, anaripotiwa kuuawa wakati wa ghasia zilizozuka nchini humo baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29.
Kwa mujibu wa maelezo ya familia yake, Ogutu hakwenda Tanzania kwa ajili ya kushiriki maandamano bali alikuwa ni mwalimu aliyefundisha katika shule moja mjini Dar es Salaam.
Katika sebule ya nyumba yao ndogo mjini Nairobi, ndugu zake Jennifer Atieno na Evans Odhiambo wameikumbatia picha ya kaka yao, nyuso zao zikijawa na huzuni.
Maumivu yanazidi kuwa makali kwa kutokujua ulipo mwili wa ndugu yao hadi sasa japo inaripotiwa kwamba mwili wake ulichukuliwa na polisi. Inaelezwa kwamba John Ogutu mara ya mwisho alisafiri hadi Kenya mnamo mwezi Julai kuhudhuria mazishi ya babake, na mara tu alipomstiri akarudi Tanzania kuendelea na kazi yake ya ualimu.
HRW yaikosoa Tanzania kwa ukandamizaji wa waandamanaji
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch lilitoa taarifa siku ya Jumanne likilaani vikali ukandamizaji wa waandamanaji kufuatia uchaguzi huo wa Oktoba 29.
Human Rights Watch ilieleza kuwa watu kadhaa waliripoti kwamba polisi walifyatua risasi ikiwalenga moja kwa moja waandamanaji.
Pia kumekuwa na madai kwamba polisi wamekuwa wakiichukua miili ya watu waliouawa wakati wa maandamano kutoka vyumba vya kuhifadhi maiti bila maelezo ya wazi, kama anavyoeleza kaka wa marehemu, Evans Odhiambo.
Odhiambo amesema familia yao imehangaika kutafuta mwili wa Ogutu bila mafanikio na wanahitaji majibu kutoka kwa mamlaka husika.
Chama Kikuu cha upinzani CHADEMA kimetoa wito wa uwajibikaji kufuatia vifo vya waliouawa katika ghasia za baada ya uchaguzi, kikidai kwamba zaidi ya watu 700 walipoteza maisha.
Afisa mwandamizi wa chama hicho anayesimamia mawasiliano ya chama na mashirika ya kimataifa, na taasisi za haki za binadamu Deogratius Munishi ameitaka mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita kuchunguza mauaji hayo.
“Tunataka uwajibikaji kwa kile kilichotokea. Tunataka kuona wale waliowapiga risasi Watanzania kwa siku sita zilizopita, wale walioua, wanawajibishwa. Na hilo lifanywe na Mahakama ya ICC na Umoja wa Mataifa na iwapo wanataka kujadiliana, basi kufanyike uchaguzi mpya unaotoa fursa kwa Watanzania kuwachagua viongozi wanaowataka.”
Hata hivyo, serikali ya Tanzania imekanusha madai ya mauaji ya watu 700, ikisema vyombo vya usalama vilifuata sheria wakati wa kudhibiti maandamano ya vurugu.