
Vituo vya kupigia kura vilichomwa moto, waandamanaji kukabiliana na polisi na hata milio ya risasi kusikika katika mitaa yote nchini humo. Licha ya hayo yote rais Samia Suluhu Hassan, aliapishwa siku chache baadae kama rais wa taifa hilo la Afrika Mashariki, baada ya Tume Huru ya Uchaguzi INEC kutangaza kwamba alishinda kwa asilimia 98 ya kura.
Miongoni mwa walioathirika na ghasia hizo ni John Okoth Ogutu, Mwalimu, raia wa Kenya aliyeishi na kufanya kazi zake huko mwa muongo mmoja.
Nyumbani mjini Nairobi, ndugu zake Jennifer Atieno na Evans Odhiambo, kile walichobakisha ni picha za kaka yao. Wana huzuni mkubwa na hofu kuwa huenda wasiuone tena mwili wa ndugu yao.
Jennifer anasema John hakwenda Tanzania kuandamana, akisisitiza kuwa ndugu yake ameishi huko kwa miaka 10 na ni mwalimu wala hakuhusika kwa namna yoyote na maandamano ya kupinga uchaguzi wa Oktoba 29. Amesema kaka yake alikuwa Kenya mwezi Julai kwa maziko ya babao na baadae akarejea nchini Tanzania.
Habari za kifo chake zilitolewa na rafiki aliyeshuhudia
Taarifa za kuuwawa kwa John zilitolewa na rafiki yake aliyeshuhudia kisa hicho. John na mwalimu mwenzake walikuwa wanakwenda nyumbani wakati walipokutana na ghasia hizo. Mwili wake unadaiwa kuuchukuliwa na jeshi la polisi. Siku kadhaa baada ya hapo hawajui mwili wa kaka yao ulipo.
Familia hiyo imesema ilipewa nafasi ya kufika katika chumba kimoja cha kuhifadhia maiti, lakini walipofika hapakuwa na dalili yoyote mwili wa ya kaka yao kuwepo huko, eneo hilo halikuwa na miili palikuwa patupu.
Hali hiyo wanasema inampa wakati mgumu sana mama yao, ambae saa nyengine anahisi kujitoa uhai, kwahiyo kila wakati anapswa kuwa chini ya uangalizi wa familia.