Mkutano kati ya Papa na Kiongozi huyo wa Palestina ulidumu kwa takriban saa moja na ulielezewa kuwa “wa kirafiki” kulingana na taarifa fupi ya Vatican. Ni mazungumzo yanayofanyika karibu mwezi mmoja tangu makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyosimamiwa na Marekani kuanza kutekelezwa katika eneo la Ukanda wa Gaza.

Papa na Abbas hawajawahi kukutana ana kwa ana. Waliwahi kuzungumza kwa simu mwezi Julai wakiangazia maendeleo katika mgogoro wa Gaza na vurugu kwenye Ukingo wa Magharibi. Kulingana na Vatican, kwenye mazungumzo haya ya leo, walijadiliana juu ya umuhimu wa misaada ya dharura kwa raia huko Gaza pamoja na kumaliza mgogoro huo kwa njia ya suluhisho la mataifa mawili.

Mnamo mwezi Septemba, Papa Leo na wanadiplomasia wake wa ngazi za juu walimwambia rais wa Israel Isaac Herzog kwamba suluhisho la mataifa mawili ndio “njia pekee ya kuvimaliza vita,” huku Vatican ikitoa wito wa usitishwaji wa kudumu wa mapigano huko Gaza. Abbas aliitembelea Vatican kuadhimisha miaka 10 ya kusainiwa kwa “Mkataba Kamili kati ya Vatican na Taifa la Palestina.”

Pamoja na mkutano huo, Abbas alikwenda kutoa heshima kwenye kaburi la Hayati Papa Francis, ambaye alikutana naye mara kwa mara huko nyuma lakini pia kuzungumza naye kwa simu mara nyingi baada ya shambulizi la Hamas nchini Israel Oktoba 7,2023 na baadae Israel ilipoivamia Gaza.

Vatican 2025 | PapaLeo XIV na Mahmoud Abbas
Kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Leo wa XIV akiwa na Kiongozi wa Mamlaka ya Palestina Mahmood Abbas Picha: Vatican Media/IPA/ZUMA/dpa/picture alliance

Taarifa nyingine kutoka Jerusalem zimesema Mamlaka za Israel zimethibitisha mapema leo kwamba mabaki ya mateka aliyerejeshwa jana Jumatano kutoka Gaza ni ya mwanafunzi Mtanzania aliyekuwa akisomea kilimo nchini Israel, ambaye aliuawa katika shambulizi hilo la Hamas la Oktoba 7, 2023.

Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ilisema mabaki hayo yalitambuliwa kuwa ni ya Joshua Loitu Mollel na familia yake imekwishaarifiwa. Mollel, mwenye umri wa miaka 21, aliwasili Kibbutz Nahal Oz siku 19 tu kabla ya shambulizi hilo, baada ya kumaliza chuo cha kilimo nchini Tanzania, na kwenda Israel kwa ajili ya kupata uzoefu zaidi.

Na taarifa za hivi karibuni zimesema Jeshi la Israel limeanzisha msururu wa mashambulizi kwenye katika maeneo ya kusini mwa Lebanon yanayokaliwa na wanamgambo wa Hezbollah, muda mfupi baada ya kuwaagiza wakazi wa maeneo hayo kuondoka.

Wakaazi waliotakiwa kuondoka ni wale wanaoishi kwenye baadhi ya majengo yaliyopo kwenye vijiji vya Aita al-Jabal, Al-Tayyiba na Tayr Debba, hii ikiwa ni kulingana na msemaji wa jeshi hilo Avichay Adraee, aliyeongeza kuwa watashambulia miundombinu ya Hezbollah, ambao wanawatuhumu kwa kujiunda upya, ikiwa ni kama mwaka mmoja tangu kufikiwa kwa makubaliano yaliyosimamiwa na Marekani ya kusitisha mapigano yalipoanza kutekelezwa baada ya miezi kadhaa ya kupigana vita.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *