Taarifa ya pamoja ya mashirika hayo imeeleza kuwa kampeni hiyo itafanyika kwa awamu tatu, Kati ya mwezi huu wa Novemba 2025 mpaka mwezi Januari 2026 ikilenga kuwapatia watoto chanjo dhidi ya magonjwa hatari kama surua, rubella, kifaduro, dondakoo, pepopunda, homa ya ini, kifua kikuu, polio na nimonia.

Awamu ya kwanza itaanza tarehe 9 hadi 18 Novemba 2025. Awamu ya pili na ya tatu za kampeni zinatarajiwa kufanyika Desemba 2025 na Januari 2026, zikiwa na lengo la kurejesha kiwango cha chanjo kama kabla ya vita.

Kabla ya vita, Gaza ilikuwa na kiwango cha chanjo cha zaidi ya asilimia 98 kwa watoto, lakini sasa kiwango cha chanjo kimeshuka chini ya asilimia 70.

Hali ikoje sasa?

Takribani mtoto mmoja kati ya watano walio chini ya miaka mitatu hajawahi kupata chanjo yoyote au amekosa dozi muhimu kutokana na vita, hali inayoongeza hatari ya milipuko ya magonjwa yanayoweza kuzuilika kwa chanjo.

Kwa mujibu wa UNICEF, kampeni hii inalenga pia kuwapima watoto hao utapiamlo na kuwapatia matibabu. “Baada ya miaka miwili ya ukatili uliogharimu maisha ya zaidi ya watoto 20,000 katika Ukanda wa Gaza, hatimaye tunayo fursa ya kuwalinda waliobaki,” amesema Jonathan Veitch, Mwakilishi Maalum wa UNICEF huko Palestina.

Veich ameongeza kuwa “Kuwachanja na kuwasaidia kiafya na kijamii watoto hawa si tu hatua ya kibinadamu bali ni wajibu wa kimaadili wa kulinda mustakabali wao.”

Watoto zaidi ya 560,000 wamepata chango ya polio katika duru ya kwanza ya kampeni ya chanjo Gaza

© UNRWA/Hussien Jaber

Kuweka sawa miundombinu

Kampeni hii itatekelezwa katika vituo 149 vya afya na magari 10 yanayotembea, huku zaidi ya wahudumu wa afya 450 na madaktari 149 wakiwa wamepewa mafunzo maalum na UNICEF, WHO na Wizara ya Afya.

WHO ina jukumu la kuratibu utekelezaji wa kampeni hiyo, ikihakikisha ubora na usalama wa huduma, pamoja na kusimamia matukio machache yanayoweza kujitokeza baada ya watoto kupatiwa chanjo.

Dkt. Richard Peeperkorn ni Mwakilishi wa WHO katika eneo la Palestina na amesema “Kampeni hii ya chanjo ni njia ya kuokoa maisha, inalinda afya za watoto na kurejesha matumaini,” ameongeza kuwa hii “Ni hatua muhimu katika kuimarisha huduma za afya na kulinda watoto waliotengwa kwa muda mrefu. Hata hivyo, kazi kubwa bado ipo tunafanya kila jitihada kujenga upya mfumo wa afya wa Gaza ili kila mtoto apate huduma anayostahili.”

UNICEF inakarabati vituo 15 vya afya, huku WHO ikikarabati vingine 20 vilivyoharibiwa. Kabla ya vita, Gaza ilikuwa na vituo 54 vya chanjo lakini sasa zaidi ya nusu ya vituo hivyo vimeharibiwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *