
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, vikwazo vya Marekani dhidi ya Wairani ni jinai dhidi ya ubinadamu.
Esmail Baghaei amesema hayo, baada ya kuhudhuria hafla ya uzinduzi wa filamu ya matukio ya kweli ya “Flight of Butterflies” ambapo amevitaja vikwazo vya kikatili vya Marekani dhidi ya Wairani kuwa ni kilele cha ukatili, unyama na jinai dhidi ya ubinadamu.
Filamu hiyo ya matukio ya kweli inasimulia maisha yenye uchungu na juhudi za kuendelea za wasomi wawili wanaougua ugonjwa wa ngozi ya kipepeo.
Esmail Baghaei alisema: “Inatosha kwamba vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran ni vya kikatili na vya kinyama kiasi kwamba wagonjwa wa ngozi ya kipepeo (EB), kama ilivyo kwa wagonjwa wengine wengi wenye maradhi yanayotibika kwa shida, daima wamekuwa katika orodha ya juu ya walengwa wa vikwazo.” Ameongeza kuwa: “Kuzuia kutumwa nchini Iran bandeji za matibabu ambazo ni maalumu kwa ajili ya wagonjwa wa EB kunaonyesha ukatili na unyama wa wawekaji na watekelezaji wa vikwazo.”
Katika miaka ya hivi karibuni, maafisa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wametahadharisha mara kwa mara kuhusu athari mbaya za vikwazo vya upande mmoja na haramu vya Marekani kwa afya za watu wakiwemo baadhi ya wagonjwa nchini Iran na kusisitiza kuwa, vikwazo hivyo vinasababisha vifo vya wagonjwa kila siku.
Licha ya madai ya Marekani kwamba hakuna vikwazo kwa vifaa vya matibabu na dawa, benki, taasisi na makampuni mengi yamekuwa na tahadhari kubwa katika kufanya biashara na Iran kwa kuhofia uwezekano wa kuadhibiwa na Marekani.