Mstaafu anakiri kwamba hakuwa miongoni mwa wananchi kadhaa waliotiki ama kutoka, hakutiki wala kutoka, kutokana na maradhi yaliyokuwa yamemshikia bango wiki ile ya kutiki ama kutoka kiasi cha kuishia kitandani hoi, wenzake wakitiki na kutoka.

Tukumbuke kwamba maradhi haya ya kiutu uzima yana kawaida ya kupamba moto kiroho mbaya yakiona mtu umeshastaafu na huna tena matibabu ya uhakika ya dezo kama ilivyo wakati umeajiriwa,

Ni kweli hakutiki wala kutoka baada ya maradhi yake ya kiutu uzima yakimtaka ashone mshono na atulize boli, pamoja na kujiona kama ameshiriki vyema kanuni muhimu hiyo ya Katiba yetu pale wahusika walipoamua kufunga mitandao yote nchini.

…Kwa wote, waliotiki na waliotoka…na sisi tulioshia kuzidi kuzeeka kitandani tukisubiri mtandao ili tuandike ‘Kona ya wastaafu’, woote tukawa nini sijui kile alichopata kusemaga Baba wa Taifa wakati fulani huko nyuma kwa kizanaki chao!

Yamepita. Tuzungumzie sasa yale yaliyomhusu mstaafu mwezi wa nane na wa tisa mwaka huu  kuhusu pensheni yake ambayo ghafla mwisho wa mwezi wa nane mstaafu anajikuta akipokea Shilingi…mama wee!…Laki nne na elfu hamsini kama pensheni yake ya mwezi mmoja inayopaswa kuwa Shilingi laki moja na elfu hamsini  kwa mwezi!

Mstaafu wetu akisema pensheni hiyo ya mwezi ya Shilingi…mama wee tena…nusu milioni haikumpa kiwewe atakuwa anasema uongo wakati anajitahidi sana uongo ukae mbali na kona ya wastaafu. Aliweweseka lakini sio kwa kupigia simu kibubu chake na benki yake kuuliza kisa cha ‘kivuno’ hicho! Aliogopa kuambiwa ‘ kiendacho kwa mganga kirudishwe fasta! Mungu sio Chesi. Haikutokea.

Tukumbuke kuwa mpaka anastaafu kazi miaka 16 iliyopita mshahara wa mstaafu wetu alioishia nao ulikuwa Shilingi laki sita na senti senti kadhaa kwa mwezi, toka mshahara wake wa Shilingi mia tatu na themanini, rudia hapo, mia, sio elfu, mia tatu themanini kwa mwezi alioanza nao kazi mwaka 1979 pale Bomani Kigoma. Makofi, tafadhali!

Alipostaafu akapokea kwanza pensheni ya elfu hamsini kwa mwezi kwa miaka kadhaa kabla ya msamaria mwema mmoja, abarikiwe, kuongeza pensheni ya wastaafu’ kwa Shilingi elfu hamsini na ikawa Shilingi laki moja na elfu tano kwa mwezi kwa miaka ishirini iliyofuta. Watu wametoka mbali ndugu zangu! Amina.

Ndio, mstaafu wetu hakuweweseka, lakini nusu milioni aliyopata kama pensheni yake ya mwezi wa nane, angalau ilimfanya aachie mdomo wazi na ahamaki…mama wee!…Pensheni ya mwezi ya Shilingi nusu milioni?

Mstaafu wetu akabaki kushangaa kama anavyoshangaaga anaposikia ama kutaja mshahara wa mwakilishi wake bungeni wa shilingi…mama wee!…milioni kumi na nne kwa mwezi, kwa kuunga mkono hoja na kushangilia kwa kupiga makofi meza, badala ya kupiga makofi wahusika wanaopanga mishahara hii!

Mstaafu akajipa natumaini kuwa inawezekana hatimaye Siri-kali ilikuwa imesikia kilio cha wastaafu’ wa kima cha chini cha kutaka waboreshewe kweli pensheni yao na imekuwa Shilingi laki nne elfu hamsini kwa mwezi ambayo inawezekana, maana wastaafu’ wenyewe wa kima cha chini wamebaki wangapi sasa!

Pensheni ya mwezi wa tisa ikawa ndogo kidogo ya Shilingi laki mbili na elfu hamsini kwa mwezi. Bado sio mbaya kama itaendelea hivyo, ndio maana hata …mama wee! …yake ilikuwa ya herufi ndogo!

Ukimya huu umemfanya mstaafu wetu arejee enzi zilee shule zilizokuwa shule kweli na mojawapo ya misemo waliyofundishwa ukawa ule wa ‘Ganda la muwa la jana, chungu kaona kivuno’!

Anaongeza maneno kidogo ili msemo uendane na wakati…’Ganda la muwa la jana, ‘chungu’ mstaafu’ ategemee kivuno chake kitadumu? Au tutarudishwa kule kule kwa laki si pesa’? Wastaafu tunaomba maelezo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *