Akihutubia huko Belém nchini Brazil kwenye mkutano wa ngazi za juu kuhusu mabadiliko ya tabianchi ambapo hii leo walikuwa na kikao cha kujadili mpito wa kuelekea kwenye nishati safi chini ya uenyekiti wa Rais Luiz Inácio Lula da Silva wa Brazil, Guterres amesema sekta ya nishati duniani inabadilika kwa kasi kubwa.

Amebainisha kuwa mwaka 2024, asilimia 90 ya uwezo mpya wa uzalishaji umeme ulimwenguni ulitokana na vyanzo vinavyoweza kurejelewa, na uwekezaji katika nishati safi ulifikia dola trilioni 2 ikiwa ni zaidi ya dola bilioni 800 kuliko uwekezaji katika mafuta ya kisukuku.

Aliongeza kuwa nishati jadidifu imekuwa chanzo cha umeme nafuu zaidi katika karibu kila nchi duniani, ikitoa ajira mara tatu zaidi kwa kila dola inayowekezwa ikilinganishwa na sekta ya mafuta ya visukuku. “Mapinduzi ya nishati jadidifu yamefika. Lakini lazima twende kwa kasi zaidi na kuhakikisha manufaa yake yanawafikia wote,”

Mambo Matano muhimu

Katibu Mkuu Guterres amesisitiza hatua tano muhimu: kuoanisha sera na sheria na mpito wa nishati safi; kuweka watu na usawa katikati ya mabadiliko; kuwekeza kwenye miundombinu ya nishati; kuhakikisha mahitaji mapya ya umeme yanakidhiwa na vyanzo safi; na kufungua uwekezaji mkubwa kwa nchi zinazoendelea.

“Leo, Afrika inapokea asilimia 2 pekee ya uwekezaji wa kimataifa katika nishati safi,” alisema Guterres. “Tunapaswa kuvunja vizuizi, kupunguza gharama za mikopo na kuvutia sekta binafsi.”

Kumbukeni ahadi zenu

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa pia alikumbusha kuwa katika mkutano wa COP28, nchi zilikubaliana kuanza mchakato wa kuachana na mafuta ya kisukuku kwa njia ya haki na mpangilio, pamoja na kutekeleza malengo ya kuongeza mara tatu uwezo wa nishati safi na kuongeza mara mbili ufanisi wa matumizi ya nishati ifikapo mwaka 2030.

Hata hivyo, alionya kuwa dunia bado ipo katika hatari kubwa, kwani hata kama ahadi zote mpya zitatekelezwa, kiwango cha joto kitazidi nyuzi 2 katika viwango vya Celsius. “Wanasayansi wanasema kuzidi kwa nyuzi 1.5 sasa hakuwezi kuepukika lakini muda na kiwango cha kuzidi huko vitategemea kasi ya hatua tunazochukua leo,” alisema.

Zama za nishati kisukuku zimekwisha

Akitamatisha hotuba yake, Guterres amesema: “Zama za mafuta ya kisukuku zinakaribia mwisho. Nishati safi inapaa. Hebu tufanye mpito huu uwe wa haki, wa haraka, na wa kudumu – ili kujenga uchumi safi, jumuishi na wenye uthabiti kwa wote.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *