
Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa kivita ICC imethibitisha mashtaka ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu dhidi ya mbabe wa kivita mtoro wa Uganda Joseph Kony bila kuwepo mahakamani.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Kony, ambaye alikuwa kiongozi wa waasi wa Lord’s Resistance Army, LRM anashtakiwa kwa makosa 39 ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu, ikiwa ni pamoja na mauaji, ubakaji, kutumia askari ambao walikuwa chini ya Umri, utumwa wa kingono na mimba ya kulazimishwa, kati ya 2002 na 2005.
Agizo la kukamatwa dhidi ya Kony lilitolewa mwaka 2005, hali ambayo ilimfanya kuwa mkimbizi wa muda mrefu zaidi wa ICC.
Majaji walitupilia mbali ombi la mawakili walioteuliwa na mahakama wanaomtetea Kony kusitisha uamuzi wa kesi hiyo na badala yake waliamua kwamba Kony anaweza kushtakiwa rasmi kwa makosa yote 39 yaliyotolewa na upande wa mashtaka.
Kando na uhalifu unaodaiwa kufanywa na wasaidizi wake, majaji walisema Kony pia anaweza kushtakiwa kwa makosa 10 ya uhalifu anaotuhumiwa kujihusisha moja kwa moja na wahasiriwa wawili ambao walikuwa wake zake wa kulazimishwa.
Kwa ajili hiyo anakabiliwa na mashtaka ya utumwa, ndoa ya kulazimishwa, mimba ya kulazimishwa, mateso kwa misingi ya umri na jinsia.
Waendesha mashtaka wamekaribisha uamuzi wa majaji na kuitaja kuwa hatua muhimu katika kumwajibisha Kony kwa uhalifu unaohusishwa naye.
Juhudi za kumsaka na kumkamata Kony, mwenye umri wa miaka 64, zinaendelea.
LRA Ilianzishwa mwishoni mwa miaka ya 1980 kwa lengo la kupindua serikali. LRA iliwatendea ukatili Waganda chini ya uongozi wa Kony kwa karibu miaka 20 Lilipopambana na wanajeshi kutoka kambi za kaskazini mwa Uganda.