Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani wimbi jipya la uchokozi wa kijeshi unaozidi kufanywa na utawala wa kizayuni wa Israel dhidi ya Lebanon, na kuikumbusha jamii ya kimataifa na nchi za kikanda kuhusu wajibu wao wa kukabiliana na uchochezi wa vita wa Tel Aviv, kwa kuuwajibisha na kuuadhibu utawala huo ghasibu.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imetoa taarifa leo Ijumaa, siku moja baada ya ndege za kivita za Israel kufanya wimbi la mashambulizi ya anga katika miji ya kusini mwa Lebanon ya Kfar Dounin, Zawtar al-Sharqiyah, Ayta al-Jabal, Taybeh, na Tayr Debba, na kuua kwa akali mtu mmoja na kuwajeruhi wengine tisa.

Wizara hiyo imeonya kuhusu matokeo hatari ya kutochukuliwa hatua utawala wa kizayuni wa Israel na kuendeleza sera zake za kivita na za kujitanua zinazolenga amani na usalama wa kikanda.

“Mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Lebanon, ambayo yamewaua shahidi na kuwajeruhi zaidi ya raia elfu moja wasio na hatia tangu yalipositishwa mapigano mwaka jana na kuharibu miundombinu na maeneo ya makazi, ni ukiukaji wa wazi wa uhuru wa kitaifa na umoja wa eneo lote la nchi huru na ni uhalifu mbaya dhidi ya amani na usalama wa kimataifa,” imeongezea taarifa hiyo.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imeeleza bayana kwa kusema: “mashambulizi haya ya kihalifu, ambayo bila shaka yanapangwa na kutekelezwa kwa usaidizi na ushirikiano kamili wa Marekani, ni ishara nyingine ya dhati ya kijinai na kigaidi ya utawala wa Kizayuni. Lengo lao pekee ni kudhoofisha uhuru na usalama wa Lebanon na kuzuia ujenzi na maendeleo ya nchi hiyo.”

Imetoa pole pia kwa Lebanon kwa kuuawa shahidi kwa raia wake wakati wa mashambulizi ya kinyama ya utawala ghasibu wa Israel.

Wakati huohuo makundi ya Muqawama ya Palestina, ikiwemo Hamas, Jihadul-Islami na Kamati za Muqawama wa Wananchi, zimelaani mashambulizi ya anga yaliyofanywa na jeshi la kizayuni dhidi ya Lebanon.

Ali Baraka, afisa mwandamizi wa Hamas, ametangaza “mshikamano kamili” na Lebanon na kutoa wito wa “kufungana safu” ili kukabiliana na uchokozi huo, akiuhimiza Umoja wa Mataifa na mataifa ya Kiarabu na Kiislamu “yatekeleze majukumu yaliyonayo haraka.”

Harakati ya Muqawama ya Ansarullah ya Yemen imesisitiza kwamba “ulegevu wa serikali ya Lebanon na kushindwa kutoa jibu kwa” mashambulizi ya mara kwa mara ya Israel ” ndiko kulikomjusurisha adui huyo.”

Katika upande mwingine, mwanadiplomasia mmoja wa Magharibi aliyeko Beirut ameonya kwamba kuendelea mashambulizi ya anga ya Israel kusini mwa Lebanon kunachochea hatari ya hakarati ya Hizbullah kutoa jibu kali la shambulio la kijeshi, kwa sababu uvumilivu ndani ya safu za harakati hiyo ya Muqawama na miongoni mwa wafuasi wake unazidi kufifia…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *