
Mashirika ya misaada ya Umoja wa Mataifa yanakabiliwa na changamoto ya kufikia maeneo yaliyotekwa na waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda tangu mwanzoni mwa mwaka, huku pia upungufu mkubwa wa ufadhili wa kibinadamu ukichangia hali hiyo mbaya. Rwanda imekanusha mara kwa mara kutoa msaada wa kijeshi kwa kundi hilo.
Cynthia Jones, Mkurugenzi wa WFP nchini DRC kwa njia ya video akiwa Kinshasa, DRC akizungumza na waandishi wa habari walio katika ofisi za Umoja wa Mataifa jijini Geniva, Uswisi, ameeleza kuwa misaada ingeweza kutolewa kwa urahisi zaidi kama njia za anga zingerejeshwa, na WFP imesisitiza, ikisema viwanja viwili vya ndege katika maeneo yanayodhibitiwa na M23 “vimefungwa kimsingi tangu mwisho wa Januari… tunatoa wito wa dharura wa kuanzishwa kwa njia ya anga ya kibinadamu.”
Tahadhari hiyo imefuatia ripoti iliyotolewa na wataalamu wa Umoja wa Mataifa wa uhakika wa chakula wakionya kuwa karibu watu milioni 25 wanakabiliwa na viwango vya juu vya ukosefu wa chakula, vinavyoainishwa kama IPC3 katika kipimo cha moja hadi tano, ambapo tano inaashiria njaa kali.
Hii inajumuisha watu milioni tatu wanaokabiliwa na viwango vya “dharura” vya njaa – IPC4 – idadi ambayo “inaongezeka kwa kasi” na “karibu mara mbili ya mwaka jana,” amesema Bi. Jones.
“Hii inamaanisha nini kwa familia? Inamaanisha kuwa wanaruka milo, wanamaliza mali zao zote za nyumbani. Wanauza mifugo yao.”
Kwa mujibu wa shirika hilo la Umoja wa Mataifa, “watu tayari wanakufa kwa njaa” katika baadhi ya maeneo ya mashariki mwa DRC.
Bi. Jones aMEbainisha kuwa mapigano kati ya waasi wa M23 na majeshi ya serikali ya DRC bado yanaendelea, na kusababisha watu wapya kukimbia, “wakilazimika kuhama makwao mara kwa mara.”
Katika mashariki mwa DRC, hali hii imesababisha watu milioni 5.2 kukosa makazi, “ikiwemo milioni 1.6 waliokimbia mwaka huu pekee, na kuifanya DRC kuwa miongoni mwa migogoro mikubwa zaidi ya watu waliokosa makazi duniani,” aliongeza afisa huyo wa WFP.
Ufadhili mdogo
Licha ya njaa kuongezeka, ufadhili wa kazi za kibinadamu unaisha, na shirika hilo limebidi kupunguza idadi ya watu wanaopokea msaada, kutoka takribani milioni moja mwanzoni mwa mwaka hadi 600,000 sasa.
“Kwa sasa tutaweza kusaidia sehemu ndogo tu ya wale wanaohitaji,” aMEsema Bi. Jones, akitoa wito wa dola milioni 350 za Marekani kusaidia chakula cha dharura na lishe katika miezi sita ijayo. “Bila fedha hizo, tutalazimika kupunguza msaada zaidi, hadi kufikia watu 300,000 pekee sawa na asilimia 10 tu ya watu milioni tatu wanaohitaji msaada.”
Bila ongezeko kubwa la fedha, WFP imeonya kuhusu “kusimama kabisa kwa msaada” kufikia Machi 2026.
“Hii inamaanisha kusitishwa kabisa kwa misaada yote ya chakula ya dharura katika mikoa ya mashariki.”
Upungufu huo mkubwa wa fedha pia umeathiri shirika hilo ndani yake. “Tunaanza kufunga ofisi zetu, kupunguza idadi ya wafanyakazi, na tunajaribu kudumisha uwezo wa kufanya kazi katika mazingira magumu sana,” ameeleza Bi. Jones.
Hata hivyo, misaada bado ni muhimu kwa watu waliokimbia katika majimbo ya mashariki ikiwemo Kivu Kaskazini, Kivu Kusini, Ituri na Tanganyika, kwani huduma muhimu zimefungwa kutokana na ukosefu wa usalama unaoendelea.
“Benki zimefungwa, hakuna pesa, na hali hii imeathiri kwa kiwango kikubwa wananchi na juhudi za kibinadamu,” alifafanua Bi. Jones. “Imearibu kabisa vyanzo vya riziki na kuweka uhakika wa chakula wa watu walioathirika katika hali mbaya sana.”
Kadri vita vinavyoendelea, familia zinatafuta hifadhi katika miji kama Ituri, ambako jamii zinazowahifadhi tayari zinateseka. Vilevile, jambo la kutia hofu ni kuwa mamilioni ya wakulima wadogo waliokimbia au wanaoogopa kurudi mashambani hawakupanda mazao msimu huu.
“Wanawake, watoto, wanaume wote wamekuwa wakipitia mateso makubwa kutokana na mfululizo wa ukatili unaofanywa na makundi yenye silaha yasiyo ya kiserikali, na kukimbia vita. Wamechoka, wamekata tamaa, wanahitaji amani,” amesisitiza Bi. Jones.