Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jordan imetangaza kuwa, inalaani vikali uamuzi wa hivi karibuni wa utawala ghasibu wa Israel wa kutangaza zabuni ya ujenzi wa vitongoji vipya 356 vya walowezi wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.

Taarifa ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jordan imesema, kutekeleza zabuni ya ujenzi wa vitongoji vipya vya walowezi wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan kunamaanisha kuimarisha uvamizi huo na ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na sheria za kimataifa za binadamu.

Sehemu nyingine ya taarifa hiyo inasema, uamuzi huo unapuuza haki isiyoweza kuondolewa ya watu wa Palestina ya kuainisha hatima yao, kukomesha ukaliaji mabavu, na kuanzisha dola huru ya Palestina ndani ya mipaka ya 1967 mji mkuu wake ukiwa Beitul-Muqaddas.

Utawala dhalimu wa Israel unaendelea kupora ardhi za Wapalestina na kuharibu nyumba zao kwa shabaha ya kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni lengo lake kuu likiwa ni kutaka kubadilisha muundo wa kijiografia wa maeneo ya Palestina na kuimarisha ukandamizaji wake katika maeneo hayo.

Katika miezi ya hivi karibuni vitendo vya hujuma na uvamizi wa walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Wapalestina hususan katika Msikiti wa al-Aqswa vimeongezeka mno.

Madola ya Magharibi yamekuwa yakikosolewa kutokana na himaya na uungaji mkono wao kwa utawala ghasibu wa Israel na hata wengi wanaamini kuwa, himaya hiyo ndiyo inayoupa kiburi utawala huo ghasibu cha kuendeleza uhharibifu na jinai zake huko Palestina.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *