Akizungumza na Idhaa ya Umoja wa Mataifa jiijni New York, Marekani, Beyani amesema wameshatoa onyo kuhusu viashiria vya mauaji ya kimbari huko El Fasher nchini Sudan na kwamba leo anakutana na mwenzake wa Muungano wa Afrika, Adama Dieng kujadili zaidi suala hilo.

Amesema, “Nadhani tutajikita kwenye uwajibikaji, ha kina aina ya mifumo ambaoy inapaswa kuanzishwa, iwe mahakama maalum au haki baada ya vita. Mashirika ya kiraia nchini Sudan nayo yametaka kuweko kwa haki na uwajibikaji ili kuepusha ukwepaji sheria ambao ndio kitovu cha ukatili unaotekelezwa Darfur.”

Pamoja na kwamba ofisi ya Beyani ilishaonya kuwa viashiria vya hatari vya uhalifu wa kikatili vipo Sudan, lakini – kama ilivyo sera ya Umoja wa Mataifa – ilisisitiza kwamba ni mahakama ya kimataifa (ICJ) au chombo cha kisheria pekee kinachoweza kubaini iwapo mauaji ya kimbari yametokea.

Msafara uliojaa familia zilizofurushwa ukikimbia El Fasher, Kaskazini mwa Darfur, kutafuta usalama. Kote Sudan, zaidi ya watu milioni 12 wamefurushwa kutoka makazi yao.

© UNICEF/Mohammed Jamal

Msafara uliojaa familia zilizofurushwa ukikimbia El Fasher, Kaskazini mwa Darfur, kutafuta usalama. Kote Sudan, zaidi ya watu milioni 12 wamefurushwa kutoka makazi yao.

Beyani ambaye ameteuliwa tu hivi karibuni kuwa Mshauri Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu kuzuia mauaji  ya kimbari, nafasi iliyoanzishwa baada ya mauaji ya kimbari nchini Rwanda, na Srebrenica,  amesema, “Tunapoangalia matukio hayo na kulinganisha na kinachoendelea hivi sasa duniani, tunaona ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, mashambulizi ya moja kwa moja dhidi ya raia, kutozingatiwa kwa sheria ya kimataifa ya kiutu ambayo inasimamia mwenendo kwenye vita. Na kwa kiasi kikubwa wanaoshambuliwa ni raia. Namaanisha tunashuhudia hali hii huko El Fasher, Sudan.”

Alipoulizwa iwapo ni vema kutangaza kuwa wanajadili kinachoendelea El Fasher kuona kama ni mauaji ya kimbari, Beyani amesema, “Kwa kuwa unapotaka kukabiliana na ukatili, ni vema kuhakikisha wanaoshiriki kwenye vita au mizozo wanafahamu kuwa wanatazamwa na wanafuatiliwa na kwamba majadiliano yanaendelea kuhusu kuzuia na uwajibikaji. Ujumbe huo unapowafikia, bila shaka, wanakuwa makini. Lakini kama kuna ukimya na ukimya, basi hicho ni kichocheo cha ukwepaji sheria.”

Kwa mujibu wa Beyani jana Alhamisi alizungumza na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan, Denise Brown, na anapanga kutoa ushauri kwa Katibu Mkuu António Guterres, Baraza la Usalama, na mfumo mpana wa Umoja wa Mataifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *