Kazi yao katika mkutano huo wa 30 wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu tabianchi, (UNFCCC) ni wazi kabisa: kubadilisha ahadi kuwa vitendo na kukubaliana juu ya mipango mikali zaidi ya kupunguza utoaji wa gesi chafuzi.
Baada ya miongo kadhaa ya ahadi na mikutano ya kila mwaka kuanzia Kyoto hadi Sharm el-Sheikh, joto ndani ya sayari dunia linazidi kuongezeka. Shinikizo kwa serikali na mashirika makubwa kuchukua hatua – si kuzungumza tu – limekuwa kubwa zaidi kuliko hapo awali.
Kwa nini COP30 inafanyika Amazon?
Kufanyika kwa COP30 huko Belém, pembezoni mwa Amazon – msitu mkubwa zaidi wa mvua wa kitropiki duniani – kunasisitiza umuhimu wa eneo hili: ni hifadhi muhimu ya kaboni na pia ni mstari wa mbele katika vita dhidi ya ukataji miti na mabadiliko ya tabianchi.
Mkutano wa mwaka huu unalenga kuongeza kasi ya utekelezaji. Wajumbe watapitia mipango ya kitaifa ya tabianchi, kusukuma ufadhili wa tabianchi wa dola trilioni 1.3 kwa mwaka, kupitisha hatua mpya za kusaidia nchi kuzoea athari za tabianchi, na kuendeleza mabadiliko ya haki kuelekea uchumi safi zaidi.
Iwe ni ukataji magogo, ukataji holela miti au mioto ya nyika, vyote hivyo vinakwamisha uwezo wa msitu wa kitropiki wa Amazoni kufyonza hewa ya ukaa ili kudhibiti madhara ya mabadiliko ya tabianchi.
“Ni wakati wa utekelezaji”
COP30 imeelezwa kama hatua ya mabadiliko – wakati wa ukweli na jaribio la mshikamano wa dunia. Mkutano huu utafunguliwa Jumatatu Novemba 10 huko Belém, huku kukiwa na hali tete kwani wanasayansi wanasema dunia iko kwenye hatari ya kupitiliza muda unaotakiwa wa kutakuwa kuhakikisha ongezeko la joto halizidi nyuzi joto 1.5 katika kipimo cha selsiyasi (1.5°C) kilichowekwa na Mkataba wa Paris mwaka 2015.
Kuzidi huko kunaweza kuwa kwa muda mfupi, wataalamu wanaonya, lakini ni ikiwa tu nchi zitachukua hatua za haraka kupunguza utoaji wa gesi chafuzi, kujiandaa kwa athari za tabianchi, na kuongeza rasilimali za kifedha.
Akizungumza katika Mkutano wa Viongozi, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema kwa uwazi: “Huu si wakati tena wa majadiliano. Ni wakati wa utekelezaji, utekelezaji na utekelezaji.”
Chini ya urais wa Brazili, COP30 itajikita kwenye ajenda ya vitendo yenye malengo 30 muhimu, kila moja ikiongozwa na “kikundi cha uanzishaji” kitakachohakikisha majawabu yanakuwa ya wigo mpana zaidi.
Juhudi hizo zimeitwa mutirão – neno la asili ya watu wa kiasili likimaanisha “kazi ya pamoja” – kuonesha azma ya Brazili ya kuangazia uongozi na ushiriki wa jamii za watu wa asili katika mkutano huu na katika mapambano ya dunia dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
Serikali inasema inataka sekta zote – kutoka kwa jamii za asili hadi viongozi wa biashara – kushiriki katika kutekeleza ahadi zilizotolewa awali kuhusu tabianchi.
Kuhamasisha fedha
Ajenda za utekelezaji katika mikutano ya COP hujengwa juu ya ahadi za hiari, si sheria za lazima. Lakini kiwango cha mabadiliko kinachohitajika ni kikubwa sana: angalau dola trilioni 1.3 za uwekezaji wa tabianchi kila mwaka kufikia mwaka 2035.
Bila hatua za haraka, wanasayansi wanaonya joto la dunia linaweza kupanda kati ya 2.3°C na 2.8°C ifikapo mwishoni mwa karne hii, na kufanya maeneo makubwa yasikalike kutokana na mafuriko, joto kali na kuharibika kwa mifumo ya ikolojia.
Kiini cha mazungumzo huko Belém kitakuwa Ripoti ya Mwelekeo kutoka Baku hadi Belém wa kusaka dola Trilioni 1.3, iliyotayarishwa na urais wa COP29 na COP30. Ripoti hiyo inaweka vipaumbele vitano vya kuhamasisha rasilimali, ikiwa ni pamoja na kuimarisha mifuko sita ya kimataifa ya fedha kukabili tabianchi, kuimarisha ushirikiano katika kodi za shughuli zinazochafua mazingira, na kubadilisha madeni ya kitaifa kuwa uwekezaji wa tabianchi – hatua ambayo inaweza kufungua hadi dola bilioni 100 kwa nchi zinazoendelea.
Ripoti hiyo pia inatoa wito wa kuondoa vikwazo kama vifungu vya mikataba ya uwekezaji vinavyoruhusu kampuni kushitaki serikali kuhusu sera za tabianchi. Migogoro kama hiyo tayari imegharimu serikali dola bilioni 83 katika kesi 349.
Nchini Liberia, kuboreshwa kwa usimamizi wa ardhi na sera za hali ya hewa zinalinda jumuiya za pwani zilizo hatarini.
Nini kingine kiko kwenye ajenda ya COP30?
Kipaumbele kingine muhimu Belém ni duru mpya ya Michango Iliyoamuliwa Kitaifa (NDCs) – mipango ya kitaifa ya tabianchi inayoeleza jinsi nchi zinavyokusudia kupunguza utoaji wa gesi chafuzi. Ili kudhibiti ongezeko la joto lisizidi 1.5°C, utoaji wa gesi duniani lazima upunguzwe kwa asilimia 60 ifikapo 2030. NDCs za sasa zinatoa punguzo la asilimia 10 pekee.
Kati ya nchi 196 wanachama wa Mkataba wa Paris, ni 64 pekee zilizokuwa zimewasilisha NDC mpya kufikia mwisho wa Septemba. Katika maandalizi yaliyofanyika Ujerumani mwezi Juni, nchi nyingi zilionya kuwa pengo hilo la matarajio lazima lifungwe katika COP30.
Wajumbe wanatarajiwa pia kupitisha viashiria 100 vya kimataifa kufuatilia maendeleo katika kuzoea mabadiliko ya tabianchi, ili matokeo yaweze kupimwa na kulinganishwa kati ya nchi.
Hadi sasa, nchi 172 zina sera au mpango mmoja wa kukabiliana na athari za tabianchi, ingawa 36 kati yake zimepitwa na wakati. Viashiria vipya vinatarajiwa kusaidia kutengeneza sera bora na wazi zaidi.
Sayari dunia ikizidi kiwango cha joto kuliko wakati wowote ule, kuchukua hatua kuhimili mabadiliko ya tabianchi ndio nguzo kuu ya hatua kwa tababichi. Lakini Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) linaonya kuwa fedha za miradi ya kuhimili mabadiliko hayo lazima ziongezwe mara 12 ifikapo 2035 ili kukidhi mahitaji ya nchi zinazoendelea.
COP30 pia itasukuma mbele Mpango wa Kazi wa Mabadiliko ya Haki – unaolenga kuhakikisha hatua kwa tabianchi haziongezi ukosefu wa usawa. Mashirika ya kiraia yanatoa wito wa kuanzishwa kwa Utaratibu wa Hatua wa Belém ili kuratibu juhudi hizo na kupanua upatikanaji wa teknolojia na fedha kwa mataifa yaliyo hatarini zaidi.
Kwa nini mikutano ya COP ni muhimu
Hapa ni mfano wa kitanda cha chuma kikiwa na nyavu moja ya mbinu ya kupandikisha matumbawe baharini katika kaunti ya kilifi nchini Kenya.
Mkutano wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC) – unaojulikana kama COP – unabaki kuwa jukwaa kuu duniani kwa ajili ya kukabiliana na janga la tabianchi. Maamuzi hufanywa kwa makubaliano ya pamoja, na hivyo kuimarisha ushirikiano katika kupunguza utoaji wa gesi chafuzi, kuzoea mabadiliko na masuala ya kifedha.
Kwa miaka mingi, mikutano ya COP imezaa makubaliano muhimu. Mnamo 2015, Mkataba wa Paris uliweka lengo la kudhibiti ongezeko la joto la dunia “lisizidi 2°C” huku ukilenga 1.5°C.
Katika COP28 huko Dubai, falme za kiarabu nchi zilikubaliana kuanza kuachana na mafuta ya kisukuku “kwa njia ya haki, yenye mpangilio na usawa,” na kuongeza uwezo wa nishati jadidifu mara tatu ifikapo 2030. Mwaka jana huko Baku, COP29 iliongeza lengo la kila mwaka la fedha za tabianchi kwa nchi zinazoendelea kutoka dola bilioni 100 hadi bilioni 300, pamoja na ramani ya njia ya kufikia dola trilioni 1.3.
Kwa ujumla, mfumo wa kisheria uliojengwa katika kipindi cha miongo mitatu chini ya UNFCCC umeisaidia dunia kuepuka ongezeko lililokadiriwa kufikia 4°C mwishoni mwa karne hii.
COP30 itaendelea hadi Ijumaa, tarehe 21 Novemba..