Kauli ya Wadephul aliyoitoa baada ya ziara yake ya hivi karibuni nchini Syria imekosolewa vikali na baadhi ya wanasiasa wakubwa wa CDU na chama dada cha CSU ambao wamekuwa wakipambana kutaka kuwarejesha kwa nguvu au kwa hiari wakimbizi wa Syria wanaoishi Ujerumani.
Alitoa kauli hiyo inayokosolewa, wakati wa mkutano wa wabunge wa vyama hivyo siku ya Jumanne. Ukosoaji huu mkali umezidi kuchochewa na chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha AfD kinachofahamika kwa siasa zake dhidi ya wageni. Umeongezewa pia nguvu na baadhi ya vitendo vya uhalifu vinavyotajwa kufanywa na wakimbizi kutoka Syria.
Jumatatu wiki hii, Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz alisema kuwa anadhani Wasyria wengi wanaweza kurejea kwao na kuongeza maneno yenye utata kuwa watakaokataa kufanya hivyo pasi na shaka wanaweza kupelekwa Syria kwa lazima
Matamshi ya Merz yalitolewa wakati kukiwa na mpasuko kwenye chama chake baada ya Johann Wadephul kusema Wasyria wanaweza kurejea nyumbani kwa kiwango kidogo sana kwa sababu sehemu kubwa ya miundombinu nchini humo imeharibiwa vibaya.
Hali katika baadhi ya maeneo ya Syria bado ni mbaya
Itakumbukwa kuwa Wadephul alizitembelea sehemu mbalimbali za mji mkuu Damascus zilizoathiriwa vibaya kwa vita.
Awali Waziri huyo wa mambo ya nje wa Ujerumani, alipokitembelea kitongoji cha Harasta mjini Damascus alisema ni vigumu kwa watu kuishi katika eneo hilo katika hali inayozingatia utu wao na kuwa wakimbizi wa Syria hawawezi kurejea katika siku za hivi karibuni.
Msemaji wa chama cha kuwatetea wakimbizi wa Syria Tareq Alaows amemtuhumu Merz kwa matamshi ya kuwatishia Wasyria kwa kuwaambia warudi nyumbani bila ya kuweka wazi ni nani atakayeathiriwa.
Itakumbukwa kuwa Ujerumani iliwapokea maelfu ya wakimbizi kutoka Syria wengi wao kati ya mwaka 2015-2016 kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe. Kati yao ni 1,000 pekee ambao wamerejea kwao kwa msaada wa serikali kwa mwaka huu. Wengine maelfu wanaoendelea kuishi Ujerumani wana vibali vya muda.