Pamba Jiji FC wataikaribisha Singida Black Stars katika kesho, Novemba 8, 2025 mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza kuanzia saa 10:00 jioni, huku wenyeji wakizitaka alama tatu za nyumbani.

Huo utakuwa mchezo wa sita kwa Pamba Jiji msimu huu, ambapo katika mechi tano zilizopita imeshinda mbili, sare mbili na kupoteza moja, huku ikifunga mabao sita na kuruhusu matano na kukamata nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikiwa na point nane.

Singida inakamata nafasi ya nane ikiwa na alama sita baada ya kucheza michezo miwili na kushinda yote dhidi ya Mashujaa FC na KMC.

Mchezo wa kesho ni wa tatu kwa timu hizo kukutana kwenye Ligi Kuu Bara, ambapo msimu uliopita Singida ilishinda 1-0 CCM Kirumba na kutoa sare ya mabao 2-2 uwanja wa Liti, Singida.

Akizungumzia maandalizi ya mchezo huo, Kocha Mkuu wa Pamba Jiji, Francis Baraza amesema vijana wake wako tayari kwa mchezo huo kwani wamefanya maandalizi ya kutosha ya kupata alama tatu nyumbani.

Amesema hana wasiwasi na ukubwa wa Singida Black Stars kwani Pamba Jiji ina historia kubwa kuliko wapinzani wao, hivyo wachezaji wakitimiza kile alichowapa mazoezini watapata ushindi.

“Tunaelewa ni mechi ngumu japo naamini wachezaji wangu wakiwa kwenye ubora wao itakuwa ni mechi nzuri. Tumewaangalia michezo yao ni timu nzuri wanakuja hapa wakiwa na ujasiri wa kuchukua alama tatu, lakini nawaambia mashabiki watarajie utakuwa mchezo mzuri,” amesema Baraza.

Kocha huyo amesema amesema nyota wake watatu akiwemo beki Abdallah Sebo ambaye ana matatizo ya kifamilia, Amosi Kadikilo na kiungo Salehe Masoud wenye majeraha watakosekana katika mchezo huo, lakini anaamini ana kikosi kipana kitakachompa matokeo mazuri.

‎“Sina hofu yoyote kama wachezaji wangu watabeba yale ambayo tumeelekazana mazoezini nina Imani tutabeba pointi tatu. Vijana wangu wako tayari nina kikosi ambacho hakinipi uoga wowote tunajua tunacheza natimu gani dakika 90 naamini zitaamua,” amesema.

‎Naye, Nahodha wa timu hiyo, Yona Amosi amesema wachezaji wako tayari kwa mchezo huo bila kujali mpinzani wanayekutana naye huku lengo likiwa ni kuwapa furaha mashabiki wao.

‎”Kwetu hakuna mechi ndogo, sisi tumejipanga niwaondoe mashaka mashabiki wa Pamba Jiji waje uwanjani hatutawaangusha. Maelekezo tunayopewa na benchi la ufundi tunayafanyia kazi kuhakikisha tunafanya vizuri,” amesema Amosi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *