
Serikali ya Marekani inasema baada ya kutathmini tena hali ya nchi na kushauriana na idara husika za Serikali ya Marekani, imebainika kuwa Sudan Kusini haikidhi tena vigezo vya kuwa katika mzozo unaoendelea ambao unatishia usalama wa raia wa Sudan Kusini wanaorejea kwao.
Ingawa kuna vurugu kati ya jamii zinazohusishwa na migogoro ya mipaka, mashambulizi ya kulipiza kisasi, na ubaguzi kwa misingi ya kikabila, inasema hakuna dalili kwa taifa hilo kuingia tena katika vita kamili vya wenyewe kwa wenyewe.
Makubaliano ya mwaka 2018 ya kuunda serikali ya Mpito ya Umoja wa Kitaifa nchini Sudan Kusini yalikusudiwa kuandaa njia ya kurejea kwa amani na uchaguzi wa kwanza kabisa wa nchi hiyo tangu uhuru wake mwaka 2011, kuundwa kwa katiba mpya, mfumo wa mahakama pamoja na uwiano wa jeshi.
Lakini, miaka 7 baadaye yote haya hayajatokea.
Nchi hiyo changa barani Afrika inakabiliwa na mvutano mwingine baada ya Rais Salva Kiir kuamuru makamu wake wa rais Riek Machar akamatwe na kushtakiwa kwa mauaji, uhaini na uhalifu dhidi ya binadamu mnamo Septemba 2025.
Raia wa Sudan Kusini sasa watatarajiwa aidha kuondoka wenyewe, kupewa tiketi ya ndege, posho ya kuondoka ya $1,000 ili kuepuka kutimuliwa kwa nguvu.
Wataalamu nchini Sudan Kusini wanasema hatua hiyo ya Marekani ya kurejesha raia wa Sudan Kusini ni njia ya kulipiza kisasi kutokana na nchi hiyo kukataa kupokea kundi la pili ya wahamiaji wa Marekani nchini Sudan Kusini.