Rais wa Kenya, William Ruto ametoa wito wa kuachiliwa kwa Wakenya wanaoripotiwa kushikiliwa nchini Ukraine, kufuatia taarifa kwamba baadhi ya vijana wa Kenya walihusishwa kinyume cha sheria katika vita vinavyoendelea kati ya Urusi na Ukraine.

Katika mazungumzo kwa njia ya simu na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, Rais Ruto alieleza wasiwasi wake kuhusu hali ya Wakenya ambao huenda walidanganywa au kulazimishwa kujiunga na mapigano hayo. Alisema viongozi hao wawili wamekubaliana kuongeza uelewa kuhusu hatari za mikakati ya ulaghai inayolenga vijana wasiojua kinachoendelea.

“Nimemuomba Rais Zelensky kusaidia kuachiliwa kwa Mkenya yeyote anayeshikiliwa nchini Ukraine. Namshukuru Mheshimiwa Rais kwa kukubali ombi langu hilo,” alisema Rais Ruto.

Rais Ruto pia alimpongeza Rais Zelensky kwa maandalizi ya Ukraine Food Summit itakayofanyika mwishoni mwa mwezi huu, na akaeleza dhamira ya Kenya kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano kati ya mataifa hayo mawili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *