Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, mauaji ya kimbari ya Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza yangali yanaendelea.
Katika ripoti iliyotolewa hivi karibuni na Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa wa haki za binadamu katika maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu Francesca Albanese, hali ya kibinadamu katika Ukanda wa Ghaza imeelezewa kuwa ni ya “mauaji dhahir ya kimbari”. Bi Albanese amesisitiza kuwa, Israel imeyapuuza makubaliano ya kusitisha mapigano na kuendelea kuwaua, kuwahamisha, na kuwatesa kwa njaa wananchi wa Palestina. Ripoti hiyo haijaashiria ukubwa tu wa mashambulizi ya kijeshi yanayofanywa na utawala wa kizayuni, lakini pia imebainihsa vitendo vya unyanyasaji wa kingono, ubomoaji wa vituo vya tiba, na kushikiliwa magerezani maelfu ya Wapalestina kunakofanywa na utawala huo ghasibu.
Albanese amesema, zaidi ya Wapalestina 200 wameuawa shahidi tangu ulipotangazwa usitishaji vita, ukiwa ni ushahidi wa namna Israel isivyoheshimu wala kujali makubaliano ya kimataifa. Kadhalika, ripota huyo maalumu wa Umoja wa Mataifa amezitaja nchi zinazoiunga mkono Israel kuwa ni washirika katika mauaji hayo ya kimbari na akatoa wito wa kuwajibishwa nchi hizo kutokana na kuupatia utawala huo wa kizayuni misaada ya silaha na uungaji mkono wa kisiasa.
Katika sehemu nyingine ya ripoti hiyo, umegusiwa pia ubomoaji uliofanywa kwa makusudi wa vituo vya tiba na hospitali. Kwa mfano, shambulio la moja kwa moja lililolenga wodi ya wazazi ya hospitali ya Al-Basma liliangamiza maelfu ya viinitete vya Wapalestina; kitendo ambacho waangalizi wa kimataifa wamekitafsiri kama jaribio la kuzuia kuendelea kuwepo kizazi cha Wapalestina.

Mbali na jinai hizo, zaidi ya Wapalestina 10,000 wangali wanashikiliwa katika jela za Israel, hali ya kuwa mateka wa Kisrael wamesharejea majumbani kwao. Ubaguzi huo wa waziwazi katika kuamiliana na mateka ni sehemu ya mfumo wa ubaguzi wa rangi wa apathaidi ambao ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa ametaka ukomeshwe.
Kadhalika, Bi Albanese amesema kuhusiana na jinsi utawala wa kizayuni unavyoamiliana na Wapalestina ya kwamba, Israel hutumia unyanyasaji wa kingono kama silaha ya kuwatishia na kuwatesea Wapalestina.
Hayo yanaripotiwa katika hali ambayo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesisitiza kwa mara nyingine tena kuhusu ulazima wa kuheshimiwa usitishaji mapigano na kuanzishwa utaratibu wa kisiasa kwa ajili ya kukomesha ukaliaji ardhi kwa mabavu na kupatiwa wananchi wa Palestina haki ya kujiamulia mustakabali wao. Guterres ametoa mjibizo pia kwa ukiukaji wa mara kwa mara wa usitishaji mapigano huko Ghaza unaofanywa na utawala wa Kizayuni na akasema: “mimi binafsi nina wasiwasi sana kutokana na ukiukaji wa usitishaji vita unaoendelea kufanywa katika Ukanda wa Ghaza.” Akizungumzia uharibifu mkubwa uliofanywa huko Ghaza, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametilia mkazo umuhimu wa kuanzishwa upya mfumo wa elimu na kurejeshwa huduma muhimu katika eneo hilo.
Onyo kali lililotolewa na Umoja wa Mataifa kuhusu kuendelea mauaji ya kimbari ya Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza yanayofanywa na jeshi la utawala wa kizayuni, sambamba na kuendelea mashambulizi dhidi ya eneo hilo lililokumbwa na maafa, vinadhihirisha dhati ya utendaji jinai uliyonayo utawala huo, ambao hata baada ya kutangazwa makubaliano ya kusitisha mapigano ungali unaendelea kuwaua Wapalestina madhulumu wa Ghaza.
Hata hivyo, licha ya maonyo hayo, muitikio wa jamii ya kimataifa ungali ni dhaifu na si wa kutosha. Hakuna shaka yoyote kwamba, utawala ghasibu wa Israel hauwezi kuendeleza jinai zake katika Ukanda wa Ghaza bila ya kupata baraka za Marekani. Na hilo amelikiri na kulithibitisha hata Rais wa nchi hiyo Donald Trump alipotoa kauli ya kushagaza kwa kusisitiza kuwa, mashambulizi yanayoendelea kufanywa na utawala wa kizayuni huko Ghaza si ukiukaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano. Katika matamshi yake ya karibuni zaidi kuhusiana na matukio ya Ghaza, Trump alitoa mjibizo kwa mashambulizi ya hivi karibuni ya Israel dhidi ya eneo hilo na kusisitiza kwa kusema: mashambulizi hayo hayajakiuka makubaliano tete ya kusitisha mapigano na kwamba “Israel ina haki ya kujilinda dhidi ya vitendo vya Hamas.” Aidha alidai, “hakuna kitu chochote kitakachohatarisha usitishaji mapigano huko Ghaza.”

Suali la kujiuliza hapa ni: kwa mtazamo wa Trump, ni hatua gani hasa ambayo utawala wa kizayuni ikiwa utachukua, utakuwa umekiuka makubaliano ya kusitisha vita vya Ghaza? Lisilo na shaka yoyote ni kwamba, kwa mtazamo wa Rais wa Marekani, endapo Hamas itachukua hata hatua ndogo kabisa ya kujihami au kutoa jibu kwa mashambulio ya kinyama ya Israel, huo utakuwa ni ukiukaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano. Uchukuaji wa msimamo huo unaonyesha kuwa, Trump hana nia ya kutoa shinikizo lolote kwa Israel ili usimamishe mashambulizi yake, kwa sababu anavyoona yeye mashambulio hayo ni mjibizo halali kwa vitisho vya kiusalama dhidi ya utawala huo wa kizayuni.
Kwa upande mwingine, kuna ripoti kadhaa zinazoeleza kwamba katika hatua za awali za mazungumzo ya kusitisha mapigano, Trump alitoa hakikisho kuwa utawala wa kizayuni utaheshimu makubaliano hayo; lakini kivitendo, na baada ya Israel kukiuka usitishaji vita, hajachukua hatua yoyote ya maana dhidi ya utawala huo.
Muelekeo huo unatafsiriwa kuwa ni uendelezaji wa sera za jadi za Marekani za kuiunga mkono Israel kwa hali yoyote ile na unaonyesha kuwa serikali ya Trump inayapa kipaumbele maslahi ya kimkakati yaliyopo baina yake na utawala wa kizayuni kuliko kusimamia bila upendeleo utekelezaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano. Na kwa muktadha huo tunaweza kusema kwamba, kutochukua hatua Trump dhidi ya ukiukaji wa makubaliano ya kusitisha vita hakutokani na udhaifu, bali ni kielelezo cha kwenda sambamba na maslahi ya pamoja ya kisiasa na kiusalama ya Washington na Tel Aviv…/