Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Rwanda, amekosoa ujumbe wa kueneza amani wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (MONUSCO) kwa kutoa mafunzo kwa wanajeshi 120 wa DRC.

Akiendeleza ukosoaji wake, katika chapisho lake jana Alkhamisi Novemba 6, 2025 kwenye mtandao wa kijamii wa X, Olivier Nduhungirehe, alidai kwamba Monusco inasaidia ukiukaji wa kusitisha mapigano kwa kusaidia jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambalo anadai lina uhusiano na kundi la FDLR (Democratic Forces for the Liberation of Rwanda), kutumia silaha nzito na ndege zisizo na rubani.

Hata hivyo, ujumbe wa kusimamia amani wa Umoja wa mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (MONUSCO) ulitangaza tarehe 4 Novemba kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba mafunzo hayo, yaliyoelezwa rasmi kuwa kwa lengo la kuongeza ulinzi wa raia na uwezo wa kijeshi, yalilenga matumizi ya ndege zisizo na rubani, utunzaji wa silaha, na mbinu za uokoaji.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imekuwa ikimtuhumu jirani yake Rwanda kuwa inaliunga mkono kundi la waasi wa M23, madai ambayo yamekanushwa na Kigali, lakini yanaungwa mkono na Marekani, Ufaransa, Ubelgiji na wataalamu wa Umoja wa Mataifa.

Rais Kagame amewahi kunukuliwa akisema kuwa, mapigano yanayoendelea, yalianzishwa na waasi waliokuwa wamekimbilia nchini Uganda, sasa hii imegeuka vipi shida ya Rwanda?  Viongozi wa waasi hao na wapiganaji wake hawana ushirikiano na Rwanda, labda tunahusishwa kwa sababu wana asili ya Rwanda, wanazungumza Kinyarwanda na huenda ndio kosa lao nchini DRC na hii imesababisha mateso yao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *