Simba imesema kuwa inahitaji kupata ushindi wa idadi nzuri ya mabao dhidi ya JKT Tanzania, kesho Jumamosi, Novemba 8, 2025 katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni, Dar es Salaam.

Kocha wa Simba, Selemani Matola amesema kuwa licha ya ubora wa wapinzani wao, wamejipanga kuhakikisha wanapata ushindi pamoja na kufunga kadri inavyowezekana ili wawe katika nafasi nzuri kwenye Ligi.

“Tumejipanga kuhakikisha tunakwenda katika mchezo huu kupata pointi tatu na kufunga bao zaidi ya moja. Hayo ndio malengo yetu ila tunafahamu mpinzani ana timu ngumu kutokana na uwepo wa wachezaji wenye uzoefu,” amesema Matola.

Beki wa Simba, Wilson Nangu amesema kuwa ushindi ndio lengo kuu katika mchezo huo.

“Wachezaji tumefanya maandalizi ya kutosha ili kwenda kushinda mechi ya kesho. Tunafahamu ugumu ambao tutakutana nao ila naamini tutakuwa bora zaidi na kutimiza lengo la kupata pointi tatu,” amesema Nangu.

Mchezo huo wa kesho, unawarudisha nyumbani wachezaji wawili wa Simba ambao msimu uliopita waliitumikia JKT Tanzania huku wakiwa tegemeo katika kikosi cha kwanza.

Wachezaji hao ni Nangu pamoja na kipa Yakoub Suleiman ambao walinaswa na Simba katika dirisha kubwa lililopita la usajili.

Simba imekusanya pointi sita katika mechi mbili za Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu dhidi ya Fountain Gate na Namungo.

JKT Tanzania imekusanya idadi ya pointi saba katika mechi tano ilizocheza dhidi ya Mashujaa FC, Coastal Union, Mbeya City, Namungo FC na Azam FC.

Hii ni mara ya tatu kwa Simba kucheza na JKT Tanzania katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo ambapo katika mara mbili zilizopita, zote Simba iliibuka na ushindi, mechi zote zikiwa ni za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *