Ni mwaka mmoja sasa tangu dikteta wa Syria Bashar Assad alipoondolewa madarakani. Lakini nchini Syria ripoti za kutisha za vurugu zinazofanywa na walinzi wa kijamii zinaendelea kugubika taifa hilo.

Kwa mfano, mwezi Oktoba, washambuliaji waliovaa mavazi meusi waliwaua kwa risasi wanaume wawili katika kijiji chenye Wakristo wengi cha Anaz kilichoko mkoa wa Homs. Washambuliaji hao walikuwa wamepanda pikipiki. Baadhi ya wachambuzi walisema mauaji hayo yalisababishwa na chuki za kidini, huku wakiitupia lawama serikali mpya ya Syria. Lakini wengine wakaangazia kile kinachotajwa “mabaki ya utawala wa Assad,” wanaotaka kuchochea migogoro ya kijamii.

Na baada ya uchunguzi zaidi ilibainika mmoja ya waliouawa ni mwanamgambo mwenye uhusiano na Assad, ambao wanadaiwa kuwaua karibu watu 700 wakati wa vita vya miaka 14 vya vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.

Vijana wengi wa Anaz, walimuunga mkono Bashar al Assad

Kulingana na gazeti la Syria la Enad Baladi, vijana wengi huko Anaz walikuwa upande wa Assad katika vita hivyo, huku kijiji kingine cha Qaalat kinachopakana na Anaz, kikiwa upande wa wanamapinduzi wanaoipinga serikali ya Syria. Ni kwa maana hiyo basi, uwezekani ni mkubwa kwamba mauaji hayo yalikuwa ni ya kulipiza kisasi.

Syria | Bado inazongwa na vurugu
Kulingana na gazeti la Syria la Enad Baladi, vijana wengi mjini Anaz walikuwa upande wa Assad katika vita vya miaka 14 vya wenyewe kwa wenyewe nchini humoPicha: REUTERS

Ghasia za walinzi hawa wa kijamii nchini Syria zinaongezeka. Katika wiki mbili za mwisho za mwezi Agosti, mwangalizi mmoja alikadiria kwamba asilimia 36 ya zaidi ya vifo 70 vya nyakati za machafuko vilikuwa ni vya mauaji ya kupangwa au mashambulizi yaliyofanywa na walinzi hao.

“Tangu utawala wa Assad ulipoondolewa madarakani Disemba 2024, serikali mpya ya mpito imeahidi kuwafikisha mbele ya sheria washirika wa utawala huo, wakiwemo watu waliofanya uhalifu wa kivita na ukiukaji wa haki za binadamu. Rais wa mpito wa Syria, Ahmad al-Sharaa, tayari amekutana na viongozi wa jamii, akiwaomba watu wawe na subira”, anasema Gregory Waters, kutoka taasisi ya sera za mahusiano ya kimataifa ya Atlantic Council yenye makao yake nchini Marekani na ambaye anafuatilia mzozo huo wa Syria.

“Hata hivyo, watu wanaikosoa mikutano hiyo, wakionekana kutokuwa na subira huku wakihoji watasubiri hadi lini?” ameongeza Gregory.

Serikali ya Ahmed al-Sharaa inapitia changamoto kuwakata wahalifu

Serikali ya Syria pia imewasamehe watu wengi waliohudumu katika jeshi la Syria, ikisema ni wale tu walio na “damu za Wasyria mikononi mwao” ndio watakaoadhibiwa kwa uhalifu wa jinai. Lakini Waters mnamo mwezi Juni aliandika juhudi za kuwakamata wahalifu hao bado zinalegalega na hazina  mwelekeo.

USA New York 2025 | Ahmed al-Sharaa
Rais wa Syria Ahmed al-Sharaa Picha: Valery Sharifulin/ITAR-TASS/IMAGO

Hadi sasa serikali ya mpito ya Syria inaonekana kana kwamba haijafanya  juhudi kubwa kushughulikia tahadhari inayotolewa dhidi ya wale wanaohusishwa na utawala wa Assad. Na bado haiko wazi ikiwa haitaki ama haina uwezo kutokana na rasilimali chache.

Kwa ujumla kuongezeka kwa mashambulizi hayo kunaonyesha jinsi mchakato unavyokwenda taratibu, anasema Mohammad al-Abdallah, mkurugenzi wa Kituo cha Haki na Uwajibikaji cha Syria chenye makao yake makuu Washington.

Kulingana naye, mamlaka hazikuwakamata wahusika wa ukiukaji na wanaendelea kuonekana mitaani. Na hii inawafanya raia kuamua kuchukua sheria mikononi kwa kuwa hawana taarifa zaidi kuhusu mpango wa serikali wa kuwawajibisha watu hawa,” al-Abdallah aliiambia DW.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *