
Idadi ya watu wanaokabiliwa na njaa mashariki ya DRC imeongezeka tangu mwaka uliopita kulingana na ripoti ya Umoja wa Mataifa.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Shirika la mpango wa chakula duniani WFP linasema idadi kubwa ya raia wanaendelea kukabiliwa na baa la njaa kwenye eneo la mashariki ya DRC.
Licha ya kwamba raia hao wanakabiliwa na uhaba wa chakula, WFP inasema imekuwa vigumu kuwahudumia wote kutokana na uhaba wa ufadhili pamoja na ugumu wa kuingia katika baadhi ya maeneo ya mashariki ya DRC.
Kulingana na Cynthia Jones, mkuu wa WFP nchini DRC, mtu mmoja kati ya watatu katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kusini, Ituri na Tanganyika wanakabiliwa na viwango vya juu wa njaa au hata zaidi.
Kwa mujibu wa mkuu huyo wa WFP nchini DRC takwimu zao zinaonyesha kwamba zaidi ya watu Milioni 10 wanakabiliwa na changamoto ya kupata chakula.
Kati ya watu hao Milioni 10, Milioni tatu wanahitaji chakula kwa dharura.
Wakati waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda kuanzisha tena uasi mwaka wa 2021, hali ya kibinadamu imekuwa mbaya zaidi mashariki ya DRC.
Hadi kufikia sasa, waasi wa M23 wameteka Miji ya Goma na Bukavu, wakiwa tena wametangaza serikali mbadala na ile ya Kinshasa pamoja na kuchukua udhibiti wa viwanja vya kuchimba madini.
WFP inasema inahitaji msaada wa dharura wa Dolla Miloni 349 kuendelea kutoa chakula cha dharura na huduma nyengine muhimu katika kipindi cha miezi sita ijayo.