
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, tangu yalipoanza kutekelezwa makubaliano ya kusitisha vita tarehe 10 Oktoba, utawala wa kizayuni wa Israel umekataa maombi 107 ya kuingizwa vifaa vya misaada katika Ukanda wa Ghaza, na hivyo kuzuia vifaa muhimu vya kibinadamu kuwafikia Wapalestina wa eneo hilo wanaoishi katika mazingira magumu na ya mateso.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Farhan Haq amewaambia waandishi wa habari: “washirika wetu wanaripoti kuwa tangu yalipositishwa mapigano, mamlaka za Israel zimekataa maombi 107 ya kuingizwa vifaa vya misaada, ikiwa ni pamoja na mablanketi, nguo na vifaa vya msimu wa baridi na vifaa vya kuendeleza na kuendesha huduma za maji, usafi wa mazingira na usafi wa mwili”.
Haq amebainisha kuwa karibu 90% ya maombi hayo yaliyokataliwa yalitoka kwa zaidi ya jumuiya 330 zisizo za kiserikali NGO’s za ndani na za kimataifa, ambapo zaidi ya nusu ya maombi hayo yalikataliwa kwa misingi kwamba mashirika hayo hayakuwa na idhini ya kupeleka vitu vya misaada huko Ghaza.
Kwa mujibu wa msemaji wa Umoja wa Mataifa, vifaa vingine ambavyo mamlaka za Israel imekataa visiingizwe Ghaza vimetolewa madai ya kuwa na aina mbili za matumizi, kuanzia magari na vipuri vyake hadi paneli za jua, baadhi ya aina za vyoo vinavyohamishika, mashine za X-ray na majenereta.
Akiinukuu Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu (OCHA), msemaji wa UN aidha amesema, matukio ya uripuaji wa majengo ya makazi yanaendelea kuripotiwa kila siku katika maeneo mengi ambako jeshi la utawala wa kizayuni lingali linaendelea kupelekwa, hususan mashariki mwa Khan Younis, mashariki mwa Jiji la Gaza na Rafah.
Huku akiashiria kuwa mashambulizi ya jeshi la Israel karibu na kile kinachoitwa “mstari wa njano” yangali yanaendelea na kusababisha maafa, Haq amesisitiza kwamba, mashambulio hayo yanahatarisha maisha ya raia, wakiwemo wafanyakazi wa ufikishaji misaada.
“Mstari wa njano” ni mstari wa kwanza wa kujiondoa ulioainishwa katika awamu ya kwanza ya makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya utawala wa kizayuni wa Israel na Harakati ya Muqawama wa Kiislamu wa Palestina HAMAS yaliyoanza kutekelezwa Oktoba 10.
Mstari huo unatenganisha maeneo ambayo yangali yako chini ya udhibiti wa kijeshi wa Israel upande wa mashariki na yale ambayo Wapalestina wanaruhusiwa kuhamia katika upande wa magharibi…/