
Dar es Salaam. Waandaaji wa mbio za kimataifa za masafa marefu (Marathoni) za Kilimanjaro Premium Lager 2026 wamewataka washiriki kujiandikisha kwa wakati kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza siku za mwisho.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana Alhamisi Novemba 6, 2025 na waandaaji hao, usajili ulianza tangu Oktoba 20, 2025.
“Hii itakuwa kwa makundi yote ya mbio, zikiwamo za kimataifa za Kilimanjaro Premium Lager kilomita 42 (mbio kamili za masafa marefu), za kilomita 21 za Yas Kili nusu marathoni) na za CRDB za kilomita tano za burudani,” inasema sehemu ya taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa Kanuni Rasmi za Riadha Duniani zinazolinda usalama wa washiriki kwa mwenyeji wa tukio, kanuni zinahitajika kuzingatiwa hasa katika usajili wa washiriki wa mbio hizo.
Kwa sasa usajili uuo utafungwa Februari 26 2026 ikiwa tiketi zitauzwa na kumalizika kabla ya tarehe iliyotajwa.
Waandaaji hao wanaeleza kuwa lengo ni kuhakikisha wanariadha wanafurahia muda wao nje ya safari bila kuwa na msongamano mkubwa, na kwamba vifaa vyote kwa upande wa maji na msaada wa matibabu unaohitajika hadi mwisho vinatayarishwa kwa ufanisi.
Kwa siku ya mbio za kimataifa za masafa marefu, waandaaji wanatoa wito kwa washiriki kuzingatia mabadiliko ya tarehe kutoka Jumapili ya mwisho ya Februari au Jumapili ya kwanza ya Machi.
Kwa sasa mbio hizo zitafanyika 22 Machi, 2026 ili waweze kupanga safari zao ipasavyo.
“Kuna wanaohitaji kushika nafasi ya malazi na kufanya maandalizi mengine, hivyo tunatoa wito kwa washiriki wote kuzingatia tarehe mpya ya toleo la mwaka ujao,” inaelezq sehemu ya taarifa ya waandalizi.
Kilimanjaro Premium Lager ndio wadhamini wakuu wa mbio za kimataifa za masafa marefu na imeshika nafasi hiyo tangu kuanzishwa kwa mbio hizo miaka 24 iliyopita.
Wadhamini wengine kwa mwaka ujao ni Yas (kilomita 21 za nusu marathoni), Benki ya CRDB kilomita 5 za burudani.
Mbio za kimataifa za masafa marefu zinaandaliwa na Kilimanjaro Marathon Company Limited kila mwaka.