Dar es Salaam. Ndilo swali la wengi baada ya kuwekwa wazi kuwa Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) kwa msimu wa 2024, zinatarajiwa kufanyika mnamo Desemba 13 mwaka huu, ukiwa ni msimu wa nne tangu zirejee.
Zuchu, staa wa Bongofleva kutokea WCB Wasafi, ndiye mwanamuziki aliyeshinda mara nyingi zaidi tangu msimu wa 2021 ambapo tuzo hizo zilirejea kwa mtindo mpya kufuatia kusimama kwa miaka saba.
Lengo kuu la tuzo za TMA ni kutambua, kuthamini na kuenzi mchango wa wasanii wa muziki nchini, pamoja na kuhamasisha ubunifu, umahiri na ushindani chanya katika tasnia ya muziki.
Kwa mujibu wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), wamedhamiria kutoa jukwaa la kipekee la kuonyesha ubunifu, ujuzi na mafanikio ya wasanii katika kukuza utamaduni, burudani na uchumi wa sanaa.
Tayari mfumo wa kupokea kazi za wasanii kwa ajili ya kushindanishwa katika vipengele mbalimbali umefunguliwa tangu Oktoba 24.
Utaratibu wa wanamuziki kujipendekeza kuwania vipengele wanavyoona wanavimudu, ulianza msimu wa 2021. Hapo awali ni kamati ya tuzo ilikaa na kupendekeza majina ya wasanii na kazi ambazo waliona zimefanya vizuri katika mwaka husika.
Msimu uliopita wa 2023, Zuchu alishinda tuzo mbili Mwimbaji Bora wa Kike Bongofleva kupitia wimbo ‘Naringa’ akiwabwaga Angella (Blessing), Appy (Watu Feki), Nandy (Falling) na Phina (Sisi Ni Wale).
Pia alishinda kipengele cha Mtumbuizaji Bora wa Kike kupitia wimbo ‘Nani Remix’ akiwabwaga Abigail Chams (Milele), Da Princess (Lolo) na Phina (Do Salale).
Kwa matokeo hayo, Zuchu akafikisha jumla ya tuzo saba za TMA, ikiwa ni baada ya msimu wa 2022 kushinda tuzo tano, na ukiwa ni msimu wake wa kwanza kushiriki.
Wakati tuzo hizo zinasimama mwaka 2015, bado Zuchu alikuwa hajatoka kimuziki na ziliporejea 2021, lebo yake ya WCB Wasafi haikuwasilisha kazi, hivyo akakosa nafasi ya kushiriki.
Kwa sasa akiwa kama kinara wa TMA tangu 2021, Zuchu ana kibarua kizito msimu huu kuendeleza rekodi yake maana wanaomkaribia wanaweza kumpita, nao ni Alikiba na Harmonize, wote wakiwa na tuzo sita.
Ikumbukwe kazi ambazo zitawania tuzo msimu huu ni zile zilizotoka mwaka 2024 pekee. Na mwaka huo, Zuchu alifanya vizuri, hivyo kuna uwezekano akashinda tena tuzo kadhaa.
Ni mwaka aliotoa albamu yake ya kwanza, Peace and Money (2024) yenye nyimbo 13 na kuwashirikisha wasanii saba akiwamo Bosi wake, Diamond Platnumz, kinara wa tuzo za MTV EMAs barani Afrika.
Kabla ya Albamu hiyo alikuwa ameshatoa nyimbo kama Zawadi (2024), Siji (2024), Pwita (2024), pamoja na Antena (2024) na Walewale (2024) ambazo pia zilikuja kujumuishwa katika albamu hiyo.
Endapo atajitosa katika kipengele cha Albamu Bora, basi washindani wake wanaweza kuwa ni Jay Melody (Therapy), Young Lunya (Mbuzi), Stamina (Msanii Bora wa Hip Hop), Marioo (The God Son), Rayvanny (The Big One) n.k
Hata hivyo, tayari Marioo amejitokeza na kudai kuwa albamu yake, The God Son (2024) ina kila sifa ya kushinda kipengele cha Albamu Bora 2024.
Msimu uliopita albamu ya Harmonize ‘Visit Bongo’ ndio ilishinda ikizibwaga nyingine kali kama ‘5’ ya Abigail Chams, ‘Swahili Kid’ ya D Voice, ‘Most People Want This’ ya Navy Kenzo na ‘Flowers III’ ya Rayvanny.
Mbali na kipengele hicho, Zuchu anaweza kuchaguliwa kuwania Mwimbaji Bora wa Kike Bongofleva, Mtumbuizaji Bora wa Kike, Video Bora ya Mwaka n.k.
Katika msimu wake wa kwanza, Zuchu alishinda Msanii Bora wa Kike wa Mwaka, Video Bora ya Mwaka, Msanii Bora wa Kike Bongofleva, Wimbo Bora wa Bongofleva na Mwanamuziki Bora wa Kike Chaguo la Watu Kidigitali.
Tuzo za TMA zilianzishwa mwaka 1999 na Basata chini ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mwaka 2003 zilipata mdhamini na kujulikana kama Kilimanjaro Tanzania Music Awards (KTMA) hadi ziliposimama 2015.
Ziliporejea tena mwaka 2022 na kuanza kuwatunza wasanii waliofanya vizuri 2021, kulikuwa na mabadiliko kadhaa ikiwamo utaratibu wa wasanii kujipendekeza, pia mwonekano wa tuzo yenyewe ambao ulikuja kubadilishwa tena msimu uliopita.