Marekani. Mama mzazi wa mwanamuziki wa Hip Hop na mfanyabiashara, Sean ‘Diddy Combs, Janice amejibu vikali madai mapya ya kisheria yanayomhusisha na biashara za zamani za mwanaye ambaye kwa sasa yupo gerezani.
Janice Combs (84), ambaye sasa anajulikana kwa jina la Janice Smalls, amewasilisha ombi mahakamani akiomba jaji kutupilia mbali kesi iliyofunguliwa na aliyekuwa mkurugenzi mtendaji wa Bad Boy Entertainment, Kirk Burrowes.
Katika kesi hiyo, Burrowes anadai kuwa Diddy alimlazimisha kusaini nyaraka za kuachia asilimia 25 ya umiliki wake wa lebo hiyo mwaka 1996, huku Janice akidaiwa kushiriki katika mpango huo.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka AllHipHop, Janice amekanusha vikali madai hayo, akisisitiza kuwa hakuhusika kwa namna yoyote ile katika tukio hilo wala katika mazungumzo ya kibiashara kati ya Burrowes na Diddy.
Pia kesi hiyo inamhusisha wakili wa muda mrefu wa Diddy, Kenneth Meiselas, kama mshtakiwa mwenza.
Burrowes aliwahi kufungua kesi kama hiyo mwaka 2003 dhidi ya Diddy na Meiselas, akidai alilazimishwa kuachia umiliki wake chini ya tishio la kupigwa, lakini kesi hiyo ilitupiliwa mbali 2006 baada ya muda wa kisheria wa kufunguliwa kuwa umeisha.
Malalamiko haya mapya yanajaribu kufufua madai hayo kwa kumhusisha Janice, jambo ambalo amelikanusha vikali.
Kesi hii inakuja baada ya mapema mwaka huu, Janice kutajwa katika kesi ya Dola33 milioni iliyofunguliwa na aliyekuwa mshirika wa karibu na Diddy, Deon ‘D1’ Best.
D1 alimshutumu Janice kwa kusaidia kuiba haki za ubunifu, mirabaha na mapato ya uandishi wa nyimbo, ikiwamo ule wa Diddy ‘Come With Me’ uliokuwa kwenye soundtrack ya filamu, Godzilla (1998).
Alidai kuwa yeye ndiye aliyemiliki, kutengeneza au kuunda wimbo huo kabla ya haki hizo kudaiwa kuchukuliwa, hatua ilipelekea kukosa mapato hayo.
Hata hivyo, kesi hiyo ilitupiliwa mbali bila kuhitimishwa rasmi. Kwa sasa, ombi la Janice kutaka kesi ya Burrowes itupiliwe nayo mbali linasubiri uamuzi wa mahakama huko Marekani.
Ikumbukwe baada ya Diddy kufukuzwa kazi Uptown Records mwaka 1993 alipokuwa msimamizi wa wasanii na vipaji, ndipo akaanzisha Bad Boy Entertainment, inayofahamika kwa jina la kibiashara kama Bad Boy Records.
Msanii wa kwanza kusainiwa na Bad Boy Records alikuwa The Notorious B.I.G., ambaye alipata mafanikio makubwa kimuziki na kibiashara baada ya kuachia wimbo wake, Juicy (1994).
Baada ya mafanikio hayo, lebo hiyo ilisaini wasanii wengine wa Hip Hop na R&B waliofanya vizuri. Wakati kilele cha mafanikio yake mwaka 1997, Bad Boy ilikadiriwa kuwa na thamani ya takribani Dola100 milioni.
Kwa sasa Diddy anatumikia kifungo cha miezi 50 gerezani baada ya kukutwa na hatia ya makosa mawili yanayohusiana na usafirishaji wa watu kwa ajili ya biashara ya ngono, hukumu iliyotolewa Oktoba 2025.