Rais Xi Jinping wa China ameitaka jamii ya kimataifa ichukue hatua kufikia usitishaji vita wa kudumu katika Ukanda wa Gaza

Katika ujumbe kwa mkutano wa Umoja wa Mataifa kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Mshikamano na Watu wa Palestina, Rais wa China alisisitiza: Jumuiya ya kimataifa inapaswa kuwajibika ili kufikia usitishaji vita wa kudumu huko Gaza.

Katika ujumbe wake Xi Jinping ameashiria kuwa suala la Palestina ndilo kiini cha migogoro ya eneo la Asia Magharibi na kusema: “Suala hili haliathiri tu uadilifu wa kimataifa, bali pia utulivu wa kikanda.”

Rais wa China amesema katika mazingira ya sasa, jamii ya kimataifa inapaswa kujenga maelewano mapana zaidi, akitoa wito wa kuchukuliwa hatua za dhati zaidi ili kuhakikisha usitishaji vita wa kina na wa kudumu huko Gaza na kuzuia kuzuka tena kwa migogoro.

Xi Jinping pia amesisitiza haja ya kuchukuliwa hatua za haraka za kuboresha hali ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza na kupunguza mateso ya watu wa Palestina.

Novemba 29 ni siku ya kimataifa ya mshikamano na watu wa Palestina.

Tarehe 29 Novemba kila mwaka hukumbusha matukio machungu yaliyojiri huko nyuma ikiwemo kuwasilishwa azimio lisilo la haki la kuigawa Palestina. Siku hii pia ni siku ya kutangaza mshikamano na wananchi wa Palestina, na ni siku ambayo Palestina ilichaguliwa kuwa mwanachama mtazamaji katika Umoja wa Mataifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *