Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amesema kuwa kulinda na kutetea umoja wa Umma wa Kiislamu ni miongoni mwa vipaumbele vikuu vya Jamhuri ya Kiislamu.

Dakta Ali Larijani ameyasema hayo katika mkutano wake na maulamaa na viongozi wa madhehebu mbalimbali za Kislamu mjini Islabad nchini Pakistan ambako alifafanua njia za kuimarisha umoja wa Kiislamu, kuunga mkono mapambano ya ukombozi wa Palestina na kupanua ushirikiano wa kiuchumi na kiusalama kati ya nchi mbili za Iran na Pakistan.

Akizungumzia juhudi za nchi za Magharibi za kuzusha migawanyiko baina ya Waislamu, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amesema: “Magharibi daima inafanya mikakati ya kuanzisha hitilafu na migawanyiko miongoni mwa Waislamu na kuibua tofauti kati ya nchi zao ili kupanua nguvu zake, na kwa sababu hiyo, viongozi wa nchi za Kiislamu, haswa viongozi wa kidini ambao wana ushawishi mkubwa katika kijamii, wanapaswa kuwa na nafasi kubwa katika kuimarisha umoja na mshikamano wa Umma wa Kiislamu.”

Amesisitiza kuwa: “Kukabiliana na sera za kuzusha hitilafu na migawanyiko za nchi za Magharibi na kuunga mkono umoja wa Umma wa Kiislamu ni miongoni mwa vipaumbele vikuu vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.”

Kwa upande wao, wasomi na viongozi wa kidini wa Pakistani pia wametilia mkazo umoja wa Umma wa Kiislamu, uungaji mkono kwa Iran na Palestina na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, kiulinzi na kikanda.

Wameashiria umuhimu wa mpango wa nyuklia wa amani wa Iran na kusema: “Mpango huo ni muhimu katika kutengeneza kinga na nguvu kwa Umma wa Kiislamu, na Iran haijawahi kutaka vita na haijaivamia nchi yoyote.”

Mkutano huo umesisitiza haja ya kuimarishwa usalama, ulinzi na maendeleo ya kiuchumi ya nchi za Kiislamu ili maadui wasiweze kutumia udhaifu wowote katika nyanja hizo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *