Ripoti iliyotolewa na Shirika la Oxfam inaonyesha kuwa, matajiri 125 wanamiliki zaidi ya utajiri wa Wakenya milioni 42.6, huku nusu ya wananchi wakiishi kwa chini ya KSh130 kwa siku.

Ripoti, hiyo iliyopewa jina, “Janga la Ukosefu wa Usawa Kenya: Mgawanyiko Mkubwa wa Kiuchumi,” inaonyesha kuwa, pengo kati ya matajiri na maskini limechochewa zaidi na ufadhili mdogo kwa sekta muhimu kama elimu, afya na kilimo.

Mwaka 2024, kati ya kila shilingi 100 iliyokusanywa kama ushuru, 68 zilitumika kulipa deni la taifa, kiasi ambacho ni mara mbili ya bajeti ya elimu na karibu mara 15 ya bajeti ya afya. Matokeo yake, watoto wanaotoka katika familia maskini hupata upungufu wa karibu miaka mitano ya masomo kuliko wale wa familia tajiri.

Matokeo hayo pia yanaonyesha kuwa ukosefu wa ufadhili wa kutosha wa elimu, afya na kilimo kwa ajili ya kutoa kipaumbele kwa ulipaji wa madeni umechangia kuongeza pengo kati ya matajiri wakubwa na wale wanaoishi katika umaskini uliokithiri.

Bei ya vyakula ni asilimia 50 juu zaidi ikilinganishwa na mwaka 2020, huku familia masikini zikiumia zaidi. Katika jiji la Nairobi, mfumuko wa bei kwa wananchi wa kipato cha chini ulikuwa asilimia 27 juu zaidi ya ule wa walio na kipato cha juu katika kipindi cha 2020–2024.

Oxfam inapendekeza mageuzi ya kodi, uwekezaji mkubwa katika elimu na afya, upanuzi wa ajira na mageuzi ya ardhi. Kwa hatua hizi, Kenya inaweza kujenga nchi iliyo sawa zaidi, yenye fursa kwa wote.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *