
Mashambulizi ya droni na makombora ya Urusi katika mji mkuu wa Ukraine wa Kyiv, yamewaua watu wawili mapema leo asubuhi. Meya wa Kyiv Vitali Klitschko alisema watu 15 walijeruhiwa, akibainisha kuwa vifusi vilivyoanguka kutoka kwenye ndege za droni, vimeharibu majengo ya makazi. Ameongeza pia kwamba maeneo ya magharibi ya mji huo yamekatika umeme.
Mashambulizi hayodhidi ya Kyiv yanafanyika wakati duru ya pili ya mazungumzo ya upatikanaji amani ikitarajiwa kufanyika.
Kulingana na afisa mmoja katika utawala wa rais wa Ukraine ambaye alizungumza kwa sharti la kutotajwa jina kwa sababu ya unyeti wa mazungumzo hayo, amesema wapatanishi wa Ukraine wanatarajiwa kukutana na wenzao wa Washington nchini Marekani wikendi hii. Kisha ujumbe wa Marekani utasafiri hadi Moscow kwa mazungumzo na Rais wa Urusi Vladimir Putin katikati ya wiki ijayo.