Dar es Salaam. Ni ukweli usiopingika kwamba mara nyingi wapenzi waliopendana wanaweza kuachana, tena katika hali ngumu na ya maumivu sana.

Katika kuachana huku wapenzi hawa wanaweza kuchukiana sana, kusemeana maneno mabaya sana, kutukanana na hata kuaibishana mbele ya wengine.

Sio kitu cha kushangaza baada ya muda mrefu au hata muda mfupi ukasikia wapenzi hawa wa zamani wanataka kurudiana au wamekwisha kurudiana na mapenzi yao yako motomoto kuliko hata mwanzoni.

Wako wengi sana wanaopata shida sana katika namna ya kuanza kumuonyesha mpenzi wa zamani kuwa anampenda na penzi limeanza kuibuka kwa upya na kwamba anatamani warudiane.

Yumkini mtu huyu anaogopa kutukanwa kwakuwa yeye ndiyo alianza kutaka waachane, au ni hofu tu ya kukataliwa baada ya maumivu makali ya kwanza. Yako makosa mengi yamekuwa yakifanywa na baadhi ya waliokuwa katika mapenzi hususani wakati mmoja anajaribu kumshawishi mwenzake ili warudiane na kuanza tena upya penzi lao.

Makosa haya yamekuwa yakitokea kwasababu ya kutofahamu nini cha kufanya na badala ya kumuweka au kumsogeza karibu na mpenzi wake wa zamani makosa haya yanamfanya kuwa mbali zaidi na kutoaminika zaidi na hivyo kuifunga kabisa milango ya uwezekano wa  kurudiana tena.

Wengi wanadhani kwa kumuahidi aliyekuwa mpenzi wako wa zamani kwamba   umebadilika  tofauti na alivyokujua zamani itasaidia.

Utafiti uliofanywa na Dk George Karanastasis mwandishi wa kitabu kinachoitwa “ How to get her back for good” umeonyesha kuwa ni ngumu sana na haifanyi kazi.

Kumwambia kuwa unampenda sana na hakuna mwingine tena baina yenu na atakayewatenganisha tena,  wala haitasaidia kuwawezesha kurudiana kiurahisi.

Ahadi nyingi unazoweza kuahidi, za ukweli na za uongo, kushawishi na hata kulia ukijitetea kuwa umebadilika na kwamba yote aliyosema umeyasikia na utayatii milele,  hayatakusaidia pia.

Mara nyingine kwa kulia sana na kuonyesha machozi kila siku jinsi ya kike huonyesha huruma mapema na kwa hivyo kijana anaweza kuhurumiwa na kujikuta wanarudiana kwa muda, lakini haitachukua muda mrefu binti aliyekubali kumsamehe kijana,  atagundua kuwa vilio na machozi yote vilikuwa usanii mtupu na hakuna kilichobadilika hata kimoja,

Hii  itakufanya kumkosa mpenzi huyu moja kwa moja, na kuifunga kabisa milango ya uwezekano wa kusamehewa tena.

Badala ya kuhangaika na jitihada zisizo zaa matunda ambazo kila siku zinamsukuma mbali unayetaka kurudiana naye, unashauriwa kufanya tofauti kabisa na kile unachofikiri kukifanya.

Kwa mfano, kamwe usijionyeshe mwenye matamanio makubwa sana ya kurudiana. Wanawake hawapendi wanaume wanaoonyesha uhitaji mkubwa sana. Wanawake hawashawishiwi wala kuchezewa akili kirahisi na kule kuomba sana au kulia kwako na kuwafanya wao wajione wana makosa na wanatakiwa kukuonea huruma ili urudi katika uhusiano.

Kujifanya mwema sana, mzuri katika kila jambo, tayari kwa kutoa msaada popote na wakati wowote,  ndilo kosa wanalofanya wanaume wengi wakidhani kwamba kwa kufanya hivyo watauweka ulimbo kumkamata kirahisi mpenzi wa zamani.

Kila siku unajigharimu kununua vitu  tele kwa ajili ya aliyekuwa mpenzi wako, huchoki kununua maua ya kila rangi ukidhani utaubadilisha moyo wake. Unajitahidi kupiga simu kila baada ya sekunde na kuuliza kama ameshakula chakula cha mchana na cha jioni.

Kila dakika huishi kutamka neno “I love you” ili tu kuonyesha kuwa siku hizi unajali kuliko zamani, wengi wamejaribu yote haya na kujikuta wanapoteza muda. Wengine wamedhani kwa kujaribu kumfanya mpenzi wake wa zamani ndiyo bosi wa maamuzi yote  ndio itasaidia.

Kwa msaada tu, kamwe usijaribu kuonyesha kana kwamba utakufa  kama mpenzi huyo hatokuwepo katika maisha yako.

Kinyume chake jaribu kujiongezea thamani  wewe mwenyewe. Yumkini wakati mpenzi wako wa zamani alipoamua kuachana na wewe,  hakuona thamani yako na thamani ya uhusiano wenu ili kumfanya abaki. Jitahidi kuonyesha thamani hiyo sasa, kama umebadilika kweli basi usiseme kwa maneno bali ishi maisha yanayoonyesha mabadiliko, wewe unajua nini kilichokuwa kinamuumiza au kumliza mara kwa mara. Kama kweli umebadilika ruhusu jamii ikuone vile ulivyobadilika, badilika kwa manufaa ya kwako mwenyewe na ya jamii nzima sio tu kwa manufaa ya mmoja unayetaka mrudiane.

Kwa kufanya hivi wala hutohangaika kumtafuta na kumfukuzia unayetamani kurudiana naye,  bali thamani yako itamfanya yeye akutafute wewe.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *