GEITA: WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde ameagiza Ofisi ya Madini mkoa Kimadini Mbogwe kufanya uchunguzi wa leseni kubwa za utafiti (PL) 191 ambazo hazijaendelezwa kwa muda mrefu.
Mavunde ametoa maagizo hayo akiwa wilayani Nyang’hwale mkoani Geita wakati wa hafla ya ugawaji wa leseni kwa vikundi vya wachimbaji wadogo iliyofanyika katika kijiji cha Nyijundu.
Amesema kabla ya uchunguzi taarifa ya awali ya leseni hizo inapaswa kuwasilishwa ofisini kwake Jumatano ya Desemba 03, 2025 ikiainisha wamiliki na mwenendo wa uendelezaji wa leseni hizo.
“Hizo leseni 191 za Geita zinafanya nini hapa, mpaka leo mkoa wa kimadini wa Mbogwe hauna mgodi mkubwa, huo utafiti wao ni wa nini, hii habari ya kushikilia maeneo ni lazima ikome”.
Mavunde amesema zoezi la kufuta leseni zisizoendelezwa ni endelevu hivo watanzania wote ambao wameshikilia maeneo ya uchimbaji bila kufanya uwekezaji wenye tija watashughulikiwa.
“Haiwezekani mtu mmoja anakalia maeneo, akigusa tu mchimbaji mdogo hapa kwangu, haiwezekani hata kidogo”, amesema na kuongeza;
“Tukitoa leseni ya utafiti, maana yake leseni ya utafiti ina miaka tisa, maliza utafiti anzisha mgodi wa kati au mkubwa, ndiyo maana ya leseni ya utafiti”, amesema Mavunde.
Mavunde amewatahadharisha wale wote wenye leseni za utafiti na wanasubiri wawekezaji ingali hawafuati kanuni na sheria za leseni hizo wajiandae kwani uchunguzi unafanyika ili kuzifuta.
Ofisa Madini Mkoa wa Kimadini Mbogwe (RMO), Jeremiah Hango amesema mbali na leseni hizo kubwa za utafiti 191 pia tayari wameshatoa leseni za uchimbaji mdogo 1,973.
Hango amekiri kuna changamoto kubwa ya maeneo mengi kushikiliwa na watu ambao wengi wao wameshindwa kufanya uendelezaji ikiwemo leseni za utafiti 191 ambazo zote hazijaendelezwa.
“Tunaomba kwenye zoezi hili ambalo linaendelea, wachimbaji wadogo ambao wameonyesha nia kubwa ya kuendelea kuchimba wapewe hayo maeneo ambayo wamiliki hawajayaendeleza”.
Katibu wa Chama Cha Wachimbaji Wadogo Geita (GEREMA), Misana Nyabange amesema PL ambazo hazijaendelezwa ndio chanzo cha migogoro kati ya wachimbaji wadogo na wawekezaji.
Mwenyekiti wa Vijana Wachimbaji wa Madini (TYM), Khamis Mohamed ameomba kanuni zitungwe ili mwekezaji atoe kipaumbele kwa vijana wanaogundua madini kwa njia za asili.
Amesema imekuwepo tabia ya wamiliki wa leseni kutumia askari kuwaondosha wachimbaji wadogo hasa vijana pale ambapo wanakuwa wamefanya ugunduzi wa madini.
